Na. Faraja Mbise, MSALATO
WANANCHI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wametakiwa kutumia haki yao ya msingi na ya kikatiba ya kupiga kura na kuchagua viongozi walio bora na wenye tija kwa maendeleo ya mitaa yao katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.
Hayo, yalisemwa na mkazi wa Mtaa wa Chikole, Glory Kondo, Kata ya Msalato, alipokuwa akifanyiwa mahojiano kuhusu muitikio wa wananchi kujitokeza kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Kuna umuhimu wa kuchagua kiongozi kwasababu ni bora ukamchagua kiongozi ambae unaona kwako wewe atakufaa kuongoza vizuri, kuliko kutokupiga kura ina maana kwamba, utakuwa umeburuzwa, unaweza ukachaguliwa kiongozi ambaye ulikuwa haumuhitaji lakini itabidi ukubaliane nae kwasababu haujajiandikisha ili kuchagua kiongozi unayemtaka. Hivyo, ni muhimu kujiandikisha na ukamchagua kiongozi unayemtaka” alisema Kondo.
Akiongolea kuhusu wananchi kujitokeza kupiga kura, alitoa wito kwa wakazi wote waliojiandikisha katika orodha ya wapiga kura kujitokeza siku ya kupiga kura na kuchagua viongozi bora na sio bora viongozi. “Wito wangu kwa waliojiandikisha ninaomba wajitokeze kuja kupiga kura. Niwajibu wao kupiga kura na kumchagua kiongozi bora kuliko bora kiongozi na wasikubali kuchaguliwa kiongozi” alisisitiza Kondo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodaboda, Tawi la Mama lililopo Msalato, Amani Howe, alizungumzia suala la maendeleo ya mitaa kuwa linajengwa na viongozi walio bora wenye kujua wajibu wao katika ngazi ya serikali za mitaa.
Kondo alisema “Ni lazima kuwe na umuhimu wa kuchagua viongozi wa mitaa kwasababu ni kuangalia maendeleo ya mitaa, endapo kama mwenyekiti aliyepita hajafanya vizuri, anaweza kuchaguliwa mwingine kwamba anaweza akabadilisha maendeleo ya mitaa yetu”
Michakato kadha wa kadha imekwisha kupita katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ikiwemo kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura, uteuzi wa wagombea wa vyama vya siasa na kukata rufaa kwa wagombea. Sanjari na hayo wananchi watapiga kura kuchagua viongozi wao wa mitaa na wajumbe wa kamati ya mtaa tarehe 27 Novemba, 2024.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.