MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amebainisha vipaumbele vinne ambavyo atavisimamia katika mkoa wa Dodoma na kusema kuwa kama watafanikiwa, Jiji la Dodoma litakuwa la kiuchúmi zaidi.
Amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na Elimu, migogoro ya Ardhi, kilimo na ufugaji venye tija na huduma bora za sekta ya afya huku akitangaza alizeti kuwa zao la biashara katika mkoa huo.
Akizungumza katika kikao kazi alichokiandaa na kuhudhuriwa na wataalam wote wa Mkoa huo chenye lengo la kuweka mikakati ili kwenda pamoja kama timu katika kutekeleza mambo yanayohusu maendeleo amesema kuwa bila kuwa na lugha moja kama Mkoa kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi itakua ngumu. "Ukitaka kufanikiwa nenda na wenzako, nawasihi tuwe na lugha ya pamoja yapo mambo mazuri wenzetu wameyafanya hivyo lazima tuyaendeleze, sisi Dodoma tunautofauti tunabeba haiba ya Makao Makuu ya nchi hivyo ni lazima tuwe na matarajio makubwa," amesema Mtaka.
Vilevile Mtaka ameziagiza Halmashauri zote nane za mkoa wa Dodoma kuwa na ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitauingizia Mkoa fedha za kutosha kuendesha miradi mbalimbali, na kuifanya kuwa ya mfano.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameelekeza kila kaya kupanda miti ili kuendeleza kampeni ya kukijanisha Dodoma ikiwa ni pamoja na wale wanaomiliki viwanja kuhakikisha kuwa wanapanda miti katika maeneo yao. "Nisisitize kila mtu awe mstari wa mbele katika kutunza mazingiza, ikiwa ni pamoja na kuacha kukata miti hovyo na badala yake tujikite katika kupanda miti katika maeneo yetu, hii iende sambamba na wenye viwanja ambao bado hawajajenga wapande miti itakusaidia kupata kivuli na hewa safi utakapohamia" alisisitiza Mtaka.
Mkutano Kazi huo wa siku moja ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Madiwani, Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, Wabunge, Wakuu wa Idara za Halmashauri, Wakuu wa taasisi zilizopo mkoani humo, na Vyombo vya Habari, ambapo pia kimehudhuriwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.