Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAKUU wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uzalendo hali wakitambua kuwa ni wasaidizi wa Rais katika wilaya zao.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka katika hafla fupi ya uapisho wa wakuu wa Wilaya wateule wa Mkoa wa Dodoma katika viunga vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma mapema wiki hii.
Mkuu wa Mkoa Mtaka alisema kuwa wakuu wa wilaya siyo wasaidizi wa Mkuu wa Mkoa bali ni wasaidizi wa Rais katika wilaya zao. “Mkijifanya ni wasaidizi wangu mtapotea.
Kila mmoja abebe thamani ya kumsaidia Rais katika wilaya yake. Hakikisheni mnatekeleza majukumu yenu kwa weledi na uzalendo mkubwa” alisema Mtaka.
Aidha, aliwapongeza wakuu wa wilaya hao kwa kuaminiwa na Rais katika nafasi hizo. Aliwataka kutambua kuwa vipaumbele katika mkoa ni elimu na viwanda. “Vipaumbele katika mkoa ni elimu na viwanda. Nendeni mkapime viwanja kwa ajili ya viwanda katika maeneo yenu. Tunataka kuitazama Dodoma katika miaka 20 ijayo tunataka kuona mabadiliko makubwa. Wekeni vivutio kwa wawekezaji ili waweze kuja kuwekeza katika maeneo yenu” alisema Mtaka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Khamis Mkanachi alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuamini na kumteua katika nafasi hiyo. Alisema kuwa kutokana na imahi hiyo atailipa kwa uwajibikaji. Akiongelea matarajio yake katika wilaya hiyo, alisema kuwa ni kuhakikisha huduma za kijamii zinakuwa bora. Aliahidi kusimamia utoaji bora wa huduma za Elimu, afya, maji, kilimo cha kisasa na uimarishaji wa uwekezaji katika sekta binafsi.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Remedius Emmanuel alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa imani aliyonayo kwake na kumuahidi ushirikiano. “Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, nikuahidi ushirikiano. Pia naomba ushirikiano wenu nyote. Kazi yangu kubwa kwenda kutekeleza imani ya Rais iliyoiweka kwa vijana inafikiwa katika Wilaya ya Kongwa” alisema Emmanuel.
Hafla hiyo ilitanguliwa na kiapo cha utii, wimbo wa Taifa, wimbo wa Afrika ya Mashariki, sala na dua na kiapo cha uadilifu kwa wateule, ilihudhuriwa na Kamati ya Usalama Mkoa, viongozi wa dini, wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wakiongozwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru na wananchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.