Tanzania kwa mara ya kwanza imethibitisha uwepo wa mgonjwa wa homa kali inayosababishwa na Virusi vya Corona.
Akitoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari leo Machi 16, 2020, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, amesema mtu huyo ni mwanamke aliyekuwa akitokea nchini Ubelgiji.
"Machi 15 tulipokea msafiri Mtanzania mwanamke mwenye umri wa miaka 46 akitokea Ubelgiji kupitia Uwanja wa Ndege wa KIA, vipimo vya awali vilionesha hana homa, baadaye alianza kujisikia vibaya na kwenda Hospitali ya Mount Meru na vipimo vya maabara vimethibitisha kuwa mtu huyu ana maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19" amesema
Amesema kuwa, mara baada ya kufika hospitalini alifanyiwa vipimo na kisha sampuli ilichukuliwa na kupelekwa maabara ya Taifa ya afya iliyopo Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi na baada ya vipimo vya maabara kufanyika vimethibitisha kuwa mtu huyo ana maambukizi ya ugonjwa wa corona (COVID-19), ambapo kwa sasa anaendelea vizuri na matibabu.
Ameongeza kuwa msafiri huyo aliondoka tarehe 3 Machi 2020, ambapo kati ya tarehe 5-13 Machi alitembelea nchi za Sweden na Denmark na kurudi tena Ubelgiji na kurejea nchini tarehe 15 Machi saa 10 jioni.
Waziri Ummy amewatoa hofu Watanzania kwa kusema Serikali imejiandaa vyema kukabiliana na ugonjwa huo huku akiwataka watu kuendelea kuchukua tahadhari zaidi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani), kuhusu kugundulika kwa mgonjwa wa Corona nchini, mkutano umefanyika Jijini Dar es Salaam, kulia ni Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tigest Katsela Mangestu na kushoto ni Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.