MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Joseph Mafuru ametoa onyo kwa wateja wa viwanja katika Jiji hilo wanaonunua maeneo mitaani bila kufuata taratibu na maelekezo ya Jiji ambalo ndiyo mamlaka ya upimaji na upangaji na uuzaji wa viwanja.
Alisema Jiji la Dodoma lina mpango kabambe tangu miaka ya 70 na umefanyiwa maboresho hivi karibuni hivyo, mwananchi atakayenunua eneo kienyeji bila kufuata sheria na taratibu anaweza kuuziwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za jamii kama makaburi kwa ajili ya kuzikia, shule au hifadhi za misitu hivyo ni vema kila anayetaka kununua kiwanja Jijini humo kufika kwenye Ofisi za Halmashauri hiyo.
Mafuru aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kikao kazi kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge na kushirikisha taasisi mbalimbali zinazohusika na uwekaji wa miundombinu mbalimbali kwenye maeneo yanayoendelezwa ikiwemo Halmashauri ya Jiji, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, Wakala ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wakala ya Barabara Mjini na Vijijini (TARURA), na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Akizungumzia upatikanaji wa viwanja kwa matumizi mbalimbali kama makazi na uwekezaji Jijini humo, Mkurugenzi Mafuru alisema Halmashauri hiyo bado ina viwanja vya kutosha vilivyopimwa katika maeneo mbalimbali hivyo kila Mtanzania anakaribishwa kununua kiwanja katika Makao Makuu ya Nchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.