MITI 780 imepandwa kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari Saba (7) wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni ya 'Mti wangu birthday yangu' iliyoasisiwa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar Mmuya na kuzinduliwa Oktoba 18, 2024, ikiwa na lengo la kuifanya Dodoma kuwa ya kijani kwa kupanda miti katika kumbukizi ya siku ya kuzaliwa.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule, imefanyika kwenye eneo la Jakaya Kikwete Square ndani ya Chuo kikuu cha Dodoma ambapo imewakutanisha wazaliwa wa mwezi Oktoba kutoka Taasisi mbalimbali, wadau wa Mazingira, wasanii na wanafunzi ambapo miti imepandwa ndani ya eneo hilo.
Akizindua Kampeni hiyo, Mhe. Senyamule amehamasisha siku za kuzaliwa ziwe maalum kwa ajili ya kupanda miti pamoja na kusisitiza Halmashauri na mtu mmoja mmoja kuzingatia agizo la upandaji miti hasa kipindi hiki cha kuelekea msimu wa mvua.
"Kutokana na juhudi za utunzaji Mazingira, mpaka sasa miti Milioni 25 imeshapandwa Mkoani humu. Kupitia Mpango huu, tunakwenda kurasimisha upandaji miti siku ya 'birthday' kwa kila mwezi na kwa maeneo maalum. Nisisitize kila Halmashauri na mtu mmoja mmoja kuanza kuandaa maeneo ya upandaji miti kukamilisha agizo la kupanda miti Milioni 1 na nusu kwa mwaka" Amesema Mhe. Senyamule
Hata hivyo, Bw. Mmuya amehimiza wananchi kupanda miti kwa wingi kadri wawezavyo na ikiwezekana kwa idadi ya miaka wanayotimiza katika mwaka husika kwani kufanya hivyo itakua faida kwa vizazi vijavyo kuepukana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
"Kuna uhusiano mkubwa kati ya wanadamu na Mazingira. Mungu alifanya miti itumie hewa chafu inayotolewa na wanadamu, nao watumie hewa safi inayotolewa na miti. Kampeni hii na nyingine nyingi zitukumbushe wanadamu juu ya uumbaji wa Mungu kwani jambo hili ni la kiibada" Mhe. Shekimweri.
Aidha, Meneja wa benki ya NMB Kanda ya kati ambaye ndiye mdhamini Mkuu wa kampeni hiyo Bi. Janeth Shango, amesema Taasisi yake itaendelea kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.