WANANCHI wa Kata ya Mtumba wamepongeza juhudi za Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Mwalimu Josephat Maganga kushuka chini ili kusikiliza na kutatua kero zao hivyo kusaidia juhudi kubwa zinazofanywa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutatua migogoro na kuboresha huduma za kijamii.
Pongezi hizo zilitolewa juzi (15/08/2020) na Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo, uliopo katika Kata ya Mtumba, Nathanael Mlunya (pichani) alipokuwa akifungua mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini kujitambulisha, kupokea na kutatua kero za wananchi wa Kata ya Mtumba.
Mlunya alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini kwa kupanga ratiba ya kutembelea Kata na kuanzia Kata ya Mtumba. “Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya nikupongeze kwa maono yako ya kuanzia Kata ya Mtumba. Nchi nzima macho yao yapo hapa Mtumba. Hivyo, uamuzi wako ni wa busara sana” alisema Mlunya.
Aidha, alimpongeza kwa kuamua kupanga ratiba ya kutembelea Kata na Mitaa kusikiliza kero za wananchi. “Napenda nikupongeze Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kwa uamuzi wako wa kushuka chini kuja kutembelea na kusikiliza kero za wananchi. Si wananchi wote wanaweza kuja mjini kuleta kero zao” alisema Mlunya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Vikonje ‘A’, Obed Mazuguni alimshukuru Rais, Dkt. John Magufuli kwa kuiona Dodoma na kulifanya kuwa Jiji zuri la kupendeza. Aidha, alipongeza kwa Mji wa Serikali kuwa katika Kata ya Mtumba na kusema imekuwa ni fursa kwa wananchi wa mtumba. “Haya mambo makubwa aliyofanya Mheshimiwa Rais, tumepata ajira na kukuza uchumi kwa wananchi wa Kata hii” alisema Mazuguni.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.