KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Utawala Bora na Serikali za Mitaa (USEMI) imetoa wito kwa Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuja na muongozo maalum utakaobainisha utekelezaji wa bajeti ya matumizi ya kawaida ya mapato ya ndani (60%) katika Idara na Vitengo za Halmashauri ili kuleta ulinganifu na usawa wa matumizi ya fedha hizo katika Halmashauri zote nchini.
"Kuna Halmashauri inakusanya mapato Bil. 4 fedha iliyotengwa katika kitengo cha Afya ni Mil. 10 nyingine inakusanya Bil.2 na imetenga zaidi ya Mil. 82 kitengo hichohicho cha Afya, ipo haja ya TAMISEMI kuandaa fomula ya matumizi ya kawaida ili idara zote ziwe na fomula moja", alisema Chaurembo
Hayo yamebainishwa Oktoba 28, 2022 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya USEMI Mhe. Jaffari Chaurembo katika kikao cha kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Bajetiya matumizi ya Kawaida (60%) kwa mwaka 2021/2022 katika Halmashauri za Rungwe, Misenyi, Longido, Kakonko pamoja na Mkinga.
Amesema kuwa kutokuwepo kwa muongozo au fomula kuna athiri utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo, akisisitiza kuwa fomula maalum itarahisisha utekelezaji wa shughuli hizo.
Baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya matumizi ya kawaida katika Halmashauri ya Kakonko, Chaurembo ameitaka Halmashauri hiyo kuwa wabunifu na kuiga mfano kutoka kwa Halmashauri nyingine katika kuibua vyanzo vya mapato ili kuondokana na dhana ya kuwa Halmashauri hiyo ni moja ya Halmashauri zinazokusanya mapato madogo nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaandaa muongozo wa utekelezaji wa Bajeti ya Matumizi ya Kawaida kwa kuzingatia mapendekezo ya kamati, Idadi ya watumishi pamoja na Jeografia ya Halmashauri husika.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.