WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema mwaka 2023 Serikali kupitia uratibu wa wizara yake inajielekeza kwenye kuimarisha na kuunganisha mifumo kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa ili kuongeza nguvu ya mapambano kwenye kudhibiti na kutokomeza ukatili wa kijinsia na watoto.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo akifungua kongamano la wanawake na uongozi lenye lengo la la kujadili ushiriki wa wanawake katika uongozi ili kutokomeza ukatili wa kijinsia, Desemba 02, 2022 jijini Dar es Salaam.
Amesema kuna haja ya kuzijengea uwezo endelevu Kamati za ulinzi wa wanawake na Watoto zilizopo ili zifanye kazi na wadau wa mitandao yote iliyoko kwenye jamii.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na Wadau inatambua umuhimu wa kuwa na wanawake viongozi mahiri na kuwekeza rasilimali katika usawa wa kijinsia kama chachu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia hivyo kamati hizo zikiimarishwa usawa wa kijinsia utafikiwa na kuondoa ukatili wa kijinsia.
Amebainisha kuwa Kamati za ulinzi wa wanawake na Watoto 18,186 kati ya 20,750 (asilimia 88) zimeanzishwa katika ngazi ya Taifa, Mkoa, Halmashauri, Kata na Kijiji kwa mwaka 2021/22.
"Tathmini ya MTAKUWWA 2017/2022 imeonesha kupungua kwa matukio ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa kwa asilimia 31 kutoka matukio 42,413 mwaka 2020 hadi 29,373 mwaka 2021. Matukio ya ukatili wa Watoto yamepungua kwa asilimia 28 kutoka matukio 15, 870 kwa mwaka 2020 hadi matukio 11,499 mwaka 2021, hata hivyo, tunatambua kuwa watu wengi bado hawatoi taarifa" amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Aidha, amebainisha kuwa katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo yenye usawa wa Kijinsia nchi inatekeleza Jukwaa la Kizazi chenye Usawa ambapo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kinara wa eneo hilo.
Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kwamba Serikali inatambua mchango mkubwa wa wanawake ambao ni zaidi ya nusu ya Watanzania wote na imeridhia mikataba mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda inayoweka misingi ya usawa kwa binadamu, ambapo matokeo ya juhudi hizo ni kuona wanawake wakishika nafasi nyeti za uongozi kwa ufanisi nchini.
Halikadhalika, amesema katika hatua hizo za maendeleo ya wanawake na uongozi anatambua mchango wa TGNP wa kufanikisha kukamilika kwa KanziData ya wanawake wenye taaluma maalum na viongozi na kuwa kinara wa kuandaa wanawake hali iliyoongeza hamasa kubwa kwa wanawake wengine kushiriki kwenye nafasi za uongozi na maamuzi.
"Kazi hizi za TGNP zinaonesha wazi jinsi gani katika maendeleo haya mchango wa wadau unachochea ajenda za serikali kwenda kasi hivyo, natoa wito kwa TGNP muendelee kuchochea ajenda hizi kwa kujipanga vizuri zaidi" amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Waziri Dkt. Gwajima amehimiza suala la ulinzi wa watoto kuanzia nyumbani hasa ufutiliaji wa mienendo yao na miili yao kwa kujenga urafiki na watoto.
Amewaomba pia Wadau kuendelea kushirikiana kupaza sauti ya kupinga ukatili sambamba na kuongezea huduma kwa manusura ambapo Kufikia Aprili 2022 jumla ya vituo vya mkono kwa mkono 21 vilianzishwa katika hospitali mbalimbali za Serikali katika Mikoa 12, Jumla ya manusura wa ukatili 1,857 walipata huduma jumuishi za matibabu, huduma za kipolisi, msaada wa kisheria na ustawi wa jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Lilian Liundi ambao ni waandaaji wa kongamano hilo amesema kuwekeza rasilimali katika usawa wa kijinsia ni kuhakikisha kuanzia sera, mipango na bajeti zinakuwa katika mlengo wa kijinsia ambapo itachangia makundi yote kunufaika katika jamii bila kuachwa mtu nyuma.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Gemma Akilimali amebainisha kuwa mabadiliko ya tabia nchi pia yanachangia kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa katika upungufu wa nishati na maji hivyo wanawake na watoto wanaathirika kwa sababu wanawake ndio watafutaji wa rasilimali hizo.
Kongamano hilo limejikita katika kujadili ushiriki wa wanawake viongozi katika kutokomeza ukatili wa kijinsia.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.