WANANCHI wametakiwa kutambua kuwa Mwanamke siyo mtu duni wala chombo cha kudhalilishwa bali anatakiwa kupewa nafasi ili naye atoe mchango wake wa kimaendeleo kadri ya uwezo wake.
Hayo yamesemwa leo machi 8, 2021 na Mbunge wa Viti maalumu, Fatuma Toufiq alipokuwa akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo yamefanyika kiwilaya katika kiwanja cha Nyerere square jijini Dodoma.
Toufiq amesema kuwa duniani kote wanawake wanafanya tathmini ya malengo ambayo wamejiwekea hususani katika kutetea haki mbalimbali za wanawake na kwamba Taifa linakabiliwa na changamoto nyingi zinazohitaji juhudi za makusudi katika kuzikabili na kwamba wenye kuweza kuzikabili changamoto hizo ni wanawake wenyewe.
Aidha, ameongeza kuwa mwanamke akipewa nafasi anaweza kwani mpaka sasa ni dhahiri wanawake waliopewa uongozi wanaweza kuongoza na kusimamia majukumu yao katika utekelezaji wa maendeleo mbalimbali.
Akifafanua zaidi, amesema kuwa kutokana na uelewa mdogo wa jamii umepelekea wanawake wengi kujiona wao si kitu si chochote lakini kutokana na juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali ya awamu ya tano imeweza kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wanawake.
"nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kumteua Makamu wa kwanza wa Rais mwanamke Mheshimiwa Samia Suluhu Hasan na kumwamini kuweza kuliongoza Taifa hili la Tanzania, hii yote ni kutimiza azma ya chachu ya kufikia Dunia yenye usawa kama ambavyo kauli mbiu ya siku ya wanawake inavyosema, nitoe rai kwa wanawake wote kutumia nafasi hii tuliyopewa katika kufanya mambo ya kimaendeleo na hasa katika kipindi hiki ambapo tayari Taifa letu lipo katika uchumi wa kati tutumie juhudi zetu na maarifa katika kuinua maendeleo yetu na hasa katika shughuli za ujasiliamali" alisema Toufiq.
Vilevile, amewataka wanawake wote kusimama imara katika kupiga vita ukatili wa kijinsia unaofanywa kwa watoto wa kike ikiwa ni pamoja na kukatishwa masomo kutokana na mimba za utotoni, kuozeshwa chini ya miaka 18, ukeketaji wa wanawake wakishirikiana na wanaume, vipigo kwa wanawake vinavyosbabishwa na jeuri ya fedha, hali inayopelekea kupoteza baadhi ya viungo na wakati mwingine kupata ulemavu wa kudumu na kupelekea mwanamke kuacha kutimiza ndoto zake.
"niwaombe wakina mama wenzangu tuongee na mabinti zetu wafahamu umuhimu wa elimu ya mimba na ndoa za utotoni, ninafahamu elimu imetolewa sana lakini tusichoke wamama sisi ndo tunajua thamani ya hawa mabinti zetu lakini pia tuendelee kuwafichua wale wote wanaowafanyia ukatili mabinti zetu ikiwa ni pamoja na kuwapa mimba wanafunzi ili waweze kuchukuliwa sheria stahiki" alisema Toufiq.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za idara ya maendeleo ya jamii jiji la Dodoma, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana, Sharifa Nabalang'anya amesema kuwa lengo la maadhimisho haya kwanza ni kutambua nafasi ya mwanamke katika jamii, pili kutoa fursa kwa wanawake, jamii na Vyama vya Siasa, Serikali na Asasi za kiraia kutafakari kwa undani mafanikio na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake katika kujiletea maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Nabalang’anya amesema kuwa katika suala la kuwawezesha wanawake kiuchumi Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeweza kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi vya wanawake vilivyokidhi vigezo ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana utegemezi.
Aidha katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 Nabalang’anya amesema kuwa Halmashauri ya jiji la Dodoma imetenga kiasi cha shilingi 2,103,848,464.00 kwa ajili ya kutoa mikopo kupitia asilimia 10 ya makusanyo ya ndani ambapo vikundi vya wanawake vilivyokidhi vigezo vitakopeshwa shilingi 840,539,380.50 kupitia asilimia nne.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.