BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeishukuru Serikali kwa kuwapa nafasi ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na ugumu wa ratiba.
Kauli hiyo imetolewa leo asubuhi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai katika zoezi la kumuombea na kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwenye uwanja wa Bunge la Tanzania.
Spika Ndugai amesema “tunaishukuru sana Serikali kwa kutupatia fursa hii ya kumuaga Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, pamoja na ratiba hii ngumu. Leo ni siku ya huzuni kubwa na majonzi makubwa. Tumechanganyikiwa, Watanzania wanalia, wamekata tamaa, lakini sisi wabunge tunasema asante Mungu kwa maisha ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye aliishi siku zote kwa kumtanguliza Mungu”.
Spika aliongeza kuwa wabunge wameondokewa na kiongozi, hasa akikumbuka mara ya mwisho alipoenda bungeni kutoa mtazamo wake kwa miaka mitano inayokuja kwa nchi ya Tanzania.
Alisema kuwa, Hayati Dkt. Magufuli aliweza kuhamisha Makao Makuu ya nchi kwenda Dodoma. “Naamini jambo hili litaendelezwa. Naamini Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Msalato utekelezaji na ujenzi wa bomba la maji kutoka Ziwa Victoria utafika Dodoma katika kumuenzi Hayati Dkt. Magufuli” alielezea imani yake Spika Ndugai.
Aidha, alimtaja kuwa amejenga barabara, viwanja vya ndege, viwanda, shule, vituo vya afya, hospitali, bwawa la kufua umeme la Nyerere. “Umejenga, umejenga, umejenga. Hii ilikuwa mbegu ya kupanda. Sisi watanzania tutahakikisha tunaitunza na kumea” alisisitiza Spika Ndugai.
Akiongea kwa huzuni kubwa, waziri mkuu wa Tanzania, Kassim majaliwa amesema kuwa Hayati Dkt. Magufuli amefanya mambo mengi ambayo hayawezi kutajwa na kumalizika haraka. “Tunachokifanya hapa ni kumuombea. Nchi nzima imegubikwa na huzuni, Afrika Mashariki na SADC. Tunashuhudia viongozi wa nchi 17 wapo hapa kumuaga, kutokana na heshima ya kiongozi wetu” amesema Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, akimuongelea hayati Dkt. Magufuli, alimtaja kuwa ndiye chimbuko lake kama Naibu Spika, alipomteua kuwa Mbunge na hatimae kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nae, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zebeir Ali Maulid, amesema kuwa Hayati, Dkt. Magufuli atakumbukwa sana kwa kazi kubwa aliyofanya. Wingi wa watu waliojitokeza kumuaga Dar es Salaam na Dodoma ni dhihirisho kuwa alikuwa ni kiongozi wa watu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.