KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2019, Mzee Mkongea Ali ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa kuboresha kituo cha Afya Mkonze kwa kujenga majengo matano mapya ya Kituo hicho, baada ya ukaguzi mapema leo na kuweka jiwe la msingi la mradi huo wa maboresho ya Kituo cha Afya.
Akiongea kabla ya kuweka jiwe la msingi, Ali alisema kuwa timu yake baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi katika Kituo cha Afya Mkonze, wamejiridhisha na ujenzi huo na kuweka jiwe la msingi. “Kituo kipo vizuri, na thamani ya fedha inaonekana. Hongereni sana” alisema Ali. Aliongeza kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kuimarisha afya za wananchi wake. Serikali imejenga vituo vya Afya 352 nchi nzima. Aidha, Serikali imeongeza bajeti ya dawa kwa Wizara ya Afya kutoka shilingi bilioni 1.9 hadi shilingi bilioni 2.2 mwaka huu” aliongeza Ali.
Akitoa ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2019, katika Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge alisema kuwa Mwenge wa Uhuru unalenga kuleta matumaini mahali ambapo hakuna matumaini, kuleta upendo mahali ambapo pana chuki na kuleta heshima mahali ambapo pana dharau.
Kiongozi huyo alisema kuwa ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 umejikita kwenye sekta ya Maji na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Aidha, aliwataka wananchi wenye sifa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu.
Awali akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi katika Kituo cha Afya Mkonze, Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho, Dkt. Baraka Chaula alisema kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa majengo matano, jengo la wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la maabara, jengo la kuhifadhi maiti na nyumba ya mtumishi.
Dkt Chaula alisema kuwa mradi ulipata fedha kiasi cha shilingi 400,000,000 kutoka Serikali kuu kwa ajili ujenzi wa majengo yote matano mapya na “Mkurugenzi wa Jiji aliongezea kiasi cha shilingi 287,826,442 zikiwa ni gharama za kufunga mfumo wa kieletroniki wa uendeshaji na kukusanyia mapato, kujenga njia za watembea kwa miguu ambazo zitaunganisha majengo, kununua vifaa mbalimbali vya kumalizia ujenzi katika majengo yote matano, mfumo wa maji taka, malipo ya ufundi, ufungaji wa mfumo wa umeme – TANESCO, malipo ya mafundi ujenzi wa kazi za ziada na ujenzi wa 'Incinarator'. Hivyo, mradi mzima utakapokamilika utagharimu kiasi cha Shilingi 687,826,442” alisema Dkt Chaula.
Mradi utakapokamilika utaongeza miundombinu mipya ya majengo, utoaji huduma za upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito, kuboresha mazingira ya kutoa na kupata huduma ya afya kwa wananchi, aliongeza. ”Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kutupa kipaumbele kuwa miongoni mwa vituo vya Afya 44 vya mwanzo kufanyiwa maboresho. Watumishi pamoja na wananchi wanafurahia kutoa na kupata huduma katika kituo hiki” alisema Dkt Chaula.
Ikumbukwe kuwa Kituo cha Afya Mkonze kilianzishwa tarehe 06/09/1993 kikiwa ni moja kati ya vituo vinne vya Afya vya Serikali vilivyopo katika Jiji la Dodoma.
Nyumba ya Mtumishi wa Kituo cha Afya ni miongoni mwa majengo ya mradi wa Maboresho ya Kituo cha Afya Mkonze.
Jengo la kuhifadhi maiti likiwa katika hatua za mwishoni kukamilika.
Jengo jipya la Maabara ya Kituo cha Afya Mkonze
Wadi ya Wazazi ya Kituo cha Afya Mkonze.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.