MWENGE wa Uhuru umeweka jiwe la msingi ujenzi wa shule ya ya mfano Ipagala baada ya kuridhishwa hatua ya ujenzi wa shule hiyo.
Jiwe hilo la msingi liliwekwa baada ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Mzee Mkongea Ali na timu yake kukagua ujenzi wa shule ya hiyo inayoendelea kujengwa katika Kata ya Ipagala.
Akiwasilisha taarifa ya mradi wa ujenzi wa shule ya msingi ya mfano, Mkuu wa idara ya Elimu ya Msingi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Joseph Mabeyo alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipokea fedha kiasi cha shilingi 706,400,000 kutoka Serikali kuu kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi mpya ya mfano. Shule hiyo itakuwa na vyumba 17 vya madarasa, bwalo la chakula, nyumba mbili za watumishi (2 in 1), maktaba moja, jengo la utawala na matundu 34 ya vyoo, aliongeza. “Majengo yote yamepauliwa na tunatarajia kukamilisha ujenzi huu mnamo tarehe 31/08/2019” alisema Mwl Mabeyo.
Akifafanua zaidi mkuu wa Idara huyo alisema Mradi huo utakapokamilika utakuwa ni shule ya mfano ambayo ina mahitaji yote muhimu kwa ajili ya Ufundishaji na ujifunzaji ili kutoa elimu bora itakayowasaidia wanafunzi kupata maarifa na ujuzi. “Shule hii itawawezesha wanafunzi kuwa mahili katika masomo hatimaye kuwa wataalam katika nyanja mbalimbali ndani na nje ya nchi na kusaidia Taifa kwenye mapinduzi ya kiuchumi yatakayo iwezesha Tanzania kuwa Nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025” aliema Mwl Mabeyo.
Kuhusu gharama za mradi, alitaja kuwa utakapokamilika mradi utagharimu shilingi 706,400,000 ambapo ujenzi wa vyumba vya madarasa 17 ni shilingi 340,000,000, bwalo la chakula moja shilingi 100,000,000 na nyumba mbili za watumishi (2 in 1) shilingi 100,000,000. Gharama nyingine ni katika ujenzi wa jengo la Maktaba shilingi 50,000,000, Jengo la utawala shilingi 50,000,000 na matundu ya vyoo 34 shilingi 37,400,000. Usafishaji wa eneo shilingi 5,000,000 na usimamizi na ufuatiliaji shilingi 24,000,000, aliongeza.
Mradi huo unafaida kwa wanafunzi, walimu na jamii iliyopo na inayozunguka Kata ya Ipagala. Faida nyingine ni kuwapunguzia umbali watoto 680 wanaosoma shule za mbali na kupunguza msongamano madarasani. Ajira kwa mafundi na vibarua ni eneo lingine ambalo ni faida kwa wananchi.
“Uwekezaji katika mradi kama huu wa elimu ni hatua muhimu katika kuzalisha nguvukazi yenye ujuzi wa kusaidia Taifa kuelekea mapinduzi ya kiuchumi. Aidha, mazingira ya shule yaliyoboreshwa huwavutia watoto kuwepo shuleni hivyo kuwawezesha kusikiliza na kufundishwa maadili mema yenyekusaidia watoto kujiepusha na tabia hatarishi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya kwa kuzingatia kaulimbiu isemayo Tujenge Maisha yetu, Jamii yetu na Utu Wetu bila Dawa za Kulevya” alisema Mwl Mabeyo.
“Tunaipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika kutekeleza sera za Chama cha Mapinduzi kwa kuendelea kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya elimu, hakika mazingira ya shule mbalimbali yameboreshwa” alisema Mwl Mabeyo. Aidha, alimshukuru kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa shule hiyo.
Baadhi ya majengo ya madarasa ya shule ya mfano.
Mkuu wa Idara ya Elimu ya Msingi wa Jiji la Dodoma Mwalimu Joseph Mabeyo akisoma taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa Shule ya mfano iliyopo Ipagala.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.