KIONGOZI wa mbio za Mwenge Maalum wa Uhuru mwaka 2021, Lt. Josephine Mwambashi amepongeza mfumo wa kieletroniki wa Udhibiti na Uendeshaji wa Vituo vya Kutolea Huduma za Afya wenye kukusanya taarifa na mapato (GOTHOMIS toleo la 4) katika kituo cha Afya Makole, jijini Dodoma kuwa wa kisasa, unaokoa muda na kwamba umesimikwa vizuri na umeleta ufanisi katika utoaji huduma.
Lt. Mwambashi alitoa pongezi hizo baada ya kukagua mfumo huo katika mbio za Mwenge maalum wa Uhuru ulipotembelea kituo hicho.
Lt. Mwambashi alisema kuwa mfumo huo ni muhimu kwa sababu unarahisisha utoaji wa huduma na kuongeza mapato. Mfumo huo unaokoa muda na kuondoa adha ya kutembea na majalada.
Kiongozi huyo baada ya kuzindua mfumo huo wa GOTHOMIS Toleo la 4, aliiagiza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kukusanya mapato kielektroniki katika vyanzo vyake vyote vya mapato.
Wakati akiwasilisha taarifa ya mfumo huo wa kieletroniki, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alisema kuwa lengo la mfumo huo lilikuwa ni kutatua tatizo sugu la upatikanaji wa taarifa mbalimbali za kituo kwa usahihi na kwa wakati.
“Lengo lingine la mfumo huu ni kuongeza usimamizi katika ukusanyaji wa mapato kituoni na uwajibikaji wa watumishi wa Afya” alisema Dkt. Method.
Akiongelea matumizi ya kaulimbiu, Dkt. Method alisema “kuna matumizi mbalimbali ya TEHAMA ambayo ni tofauti na mfumo. Mfano, mashine ya kusaini mahudhurio kwa alama za vidole imesaidia katika uwajibikaji hasa kuwahi kazini kwa watumishi na kudhibiti muda wa kazi/ kutoka. Mfumo wa FFARS katika utumiaji wa fedha kituoni, hivyo imesaidia kufanya matumizi kwa usahihi na CCTV camera zilizofungwa kituoni zinasaidia katika kuongeza ulinzi”.
Kituo cha Afya Makole kilianzishwa mwaka 1978 kikiwa ni moja kati ya vituo vinne vya Afya vya serikali vilivyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kikiwa na majengo 10.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.