WAZIRI mkuu mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Kayanza Pinda amepongeza utendaji kazi unaofanywa na Rais Dkt. John Magufuli katika mapambano dhidi ya rushwa na kurudisha nidhamu kwa watumishi wa umma nchini.
Pongezi hizo alizitoa alipokuwa akitoa salamu kufuatia Mwenge wa Uhuru kutembelea shamba lake eneo la Zuzu (Nzinje) kuzindua mradi wa ufugaji Samaki.
Pinda alisema ”shukrani kwa Rais Dkt John Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya. Nimefanya kazi na tawala zote. Rais Magufuli ameonesha jeuri isiyo ya kawaida katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Katika utawala wake nidhamu imerudi kwa watendaji serikalini”. Maeneo mengine yaliyofanywa na Serikali hii aliyataja kuwa ni ujenzi wa mradi mkubwa wa bwawa la kufua umeme la Nyerere na reli ya kisasa ya umeme.
Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Mzee Mkongea Ali alimpongeza waziri mkuu mstaafu na kumuita mzalengo wa kweli. ”Katika eneo hili, watu mbalimbali wamekuwa wakija kujifunza shamba darasa bure, huu ni uzalengo wa kweli” alisema Ali. Kiongozi huyo Mzee Mkongea Ali amezindua rasmi Shamba hilo la Samaki katika eneo la Zuzu, Shamba linalomilikiwa na Pinda Farm Products ya Waziri Mkuu mstaafu Mhe. Mizengo Peter Kayanza Pinda.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi wa ufugaji Samaki katika shamba la Pinda, Mama Tunu Pinda alisema kuwa mradi wa ufugaji Samaki katika shamba la waziri mkuu mstaafu ni miongoni mwa miradi michache ya ufugaji Samaki iliyopo mkoani Dodoma, ukiwa na ujenzi wa mabwawa saba. Alisema kuwa mradi huo umegharimu shilingi milioni 29,500,000 kwa kujenga mabwawa saba.
Akiongelea aina ya Samaki wanaozalishwa katika shamba hilo, alisema kuwa shamba hilo linazalisha Sato na Kambale. “Kwa upande wa Samaki aina ya Sato, bwawa dogo moja lina idadi ya Samaki kati ya 2,500 hadi 4,000. Bwawa kubwa lina idadi ya Samaki kati ya 8,000 hadi 10,000. Kwa upande wa Samaki aina ya Kambale bwawa dogo linachukua Samaki 10,000 na bwawa kubwa linachukua Samaki 30,000. Mpaka sasa tumeshavua Samaki 1,800 kwa ajili ya kuuza awamu ya kwanza. Jumla ya Samaki waliopo ni 6,000 Kambale pamoja na Sato. Kwa wastani bei ya Samaki ni shilingi 9,000 kwa kila kilo moja” alisema mama Pinda.
Mama Pinda aliendelea kusema kuwa ufugaji Samaki unakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa chakula cha Samaki cha uhakika kwa bei nafuu ndani ya nchi. ”Kwa sasa chakula kinachopatikana kinatengenezwa nje ya nchi na kuuzwa kwa bei kubwa. Vifaranga vya samaki hupatikana maeneo ya mbali kama mto Ruvu ulioko Mkoa wa Pwani ambapo usafirishaji wake unakuwa mgumu mpaka kufika Dodoma vifaranga wengine wanakuwa wamechoka au wamekufa” alisema mama Pinda.
Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda akitoa maelezo kuhusu mabwawa ya Shamba la Samaki kwa wakimbiza Mwenge wa Uhuru 2019.
Mandhari ya eneo la Shamba la Samaki la Mzee Mizengo Pinda.
Baadhi ya samaki aina ya sato wanaopatikana kwenye Shamba la Samaki linalomilikiwa na Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda Kayanza Pinda.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.