MWENYEKITI wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Naghenjwa Kaboyoka amesema wamekuwa wakifanya kazi na WAJIBU kwa karibu sana na kwamba WAJIBU wamekuwa kama Bunge nje ya Bunge, wamekuwa wakiwakilisha wananchi, maana hizo ripoti zao wanazichambua kiasi kwamba wananchi wanaweza kuzisoma na kuzielewa.
Hayo ameyasema wakati wa uzinduzi wa Ripoti za Uwajibikaji ambazo zimetokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) Jijini Dodoma na kuandaliwa na Taasisi ya WAJIBU ili kuwarahisishia wananchi kuzisoma kwa wepesi.
Kaboyoka amesema "Kwa hiyo WAJIBU imekuwa mkono wetu wa kulia wa kusaidia kamati zetu mbili za PAC na LAAC, unakuta wenzetu wanakwenda mbali zaidi kueleza yale ambayo hatupati muda wa kuyazungumzia bungeni lakini wenzetu WAJIBU wanayachambua na kuyaeleza kwa wadau, na hivyo wadau wanapata nafasi ya kujua kilichopo.
Kwa mfano tukiangalia bajeti ya mwaka huu siku zote tunasema kilimo ndio uti wa mgongo lakini ukiangalia bajeti iliyopita nafikiri ilitolewa asilimia mbili tu na hii ndio sekta ya uzalishaji, sasa kama sekta ya uzalishaji haitatengewa hela nyingi zikazalisha tunategemea maendeleo gani? yatakuwa maendeleo ya vitu sio watu.
Serikali za Mitaa tuna tatizo moja, inawezekana hawa wenzetu tangu wamemaliza shule hajawahi kupelekwa kozi, hajui tena taratibu za kimataifa za kutoa ripoti zimekuaje, matokeo yake inawezekana kweli hajaiba lakini akawa hajui jinsi ya kuandaa ripoti, kwa hiyo anapata ripoti chafu.
Lakini kusema kweli ni vizuri hawa wenzetu ambao wapo katika taaluma ya kusimamia masuala ya fedha mara kwa mara wapelekwe kwenye kozi, waelezwe taratibu mpya na kufundishwa, maana utakuta wanasema hawa wamezoea kuandika vocha tu," amefafanua kwa upana Mhe. Kaboyoka.
Ameongeza kuwa inawekana ni wasomi wazuri lakini viwango vya kimataifa vya kuandaa ripoti ambavyo vimewekwa havijui, hivyo halmashauri inapata hati chafu, mwingine anapata hati safi na anayepata hati safi haina maana mambo yao ni mazuri kuliko aliyepata hati chafu. "Lakini ina maana gani, hesabu zao hawajazifunga kwa utaratibu unaokubalika kimataifa".
Aidha amesema anashukuru kusikia kuna halmashauri ambazo zimeanza kuchukua hatua za kuwapeleka watu wao wa kuandaa ripoti kupata kozi za kuwaongezea ujuzi huku akieleza CAG anaweza kusaidia hao watu wakaelekezwa namna ya kufunga hesabu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.