NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba ametoa siku 60 kwa mkandarasi SUMA-JKT kukamilisha ujenzi wa tenki la maji la Buigiri – Chamwino litakalogharimu kiasi cha shilingi milioni 998 linatarajiwa kuhudumia wakazi wa Chamwino na Hospitali ya Rufaa ya Uhuru jijini Dodoma.
Mhandisi Kemikimba ametoa agizo hilo leo alipofanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa tenki hilo litakalokuwa na ujazo wa lita milioni mbili na laki tano lililoko eneo la Buigiri–Chamwino.
“Tumekubaliana na mkandarasi kuwa tenki hili likamilike ndani ya mwezi wa pili, kwa hiyo wana siku 60 tu kuhakikisha ujenzi umekamilika” alisema.
Aidha, ameitaka menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Dodoma (DUWASA) kufanya ufuatiliaji wa ujenzi wa tenki hilo kila siku ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu Kemikimba ametembelea eneo la Ihumwa panapochimbwa visima na amekiagiza kitengo cha uchimbaji kilicho chini ya RUWASA kuongeza kasi ya uchimbaji visima ili kukamilisha miradi kwa wakati lengo ikiwa ni kuongeza kiasi cha maji kwa Jiji la Dodoma.
Akiwa katika eneo la Nzuguni, Naibu Katibu Mkuu, Kemikimba amekagua kazi inayoendelea ya flushing ya kisima itakayosaidia kuongeza kiasi cha maji kwa Jiji la Dodoma na amesema kuwa ameridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) kwa kuwa wabunifu katika kutafuta vyanzo vya maji.
Ziara hizo ni muendelezo wa ziara zake za kukagua utekelezaji wa miradi ya maji katika Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.