Na. Getruda Shomi na Sifa Stanley, DODOMA
NAIBU Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mhe. Emmanuel Chibago amehamasisha Mashirika binafsi na Serikali kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kutoa misaada mbalimbali kwa jamii ikiwemo watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu ili kuweza kukwamua jamii kutoka kwenye umaskini na kujenga uchumi.
Mhe. Chibago ameyasema hayo alipohudhuria mkutano wa kufunga Mradi wa Kizazi Kipya uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Dodoma na kuona namna mradi huo ulivyofanya kazi kwa muda wa miaka mitano.
Naibu Meya huyo amesema kuwa wadau wa maendeleo na Serikali waendelee kuiendeleza miradi ambayo inaanzishwa na Mashirika binafsi. “Naomba tuendeleze mradi, walipotufikisha tuendelee mbele, ikiwemo Halmashauri na wadau wetu, niwaombe tunayoyafanya haya tuyafanye kwa moyo mmoja. Tuendelee kuzifanya kazi hizi ni za kujitolea” amesema Chibago.
Meneja wa Mradi wa Afya ya Mama na Mtoto wa Shirika la World Vision, Daud Gambo aliongeza kuwa wadau, serikali na jamii kwa ujumla waendelee kushirikiana ili kuhakikisha wanaikomboa jamii kutoka kwenye umaskini “tushikane mikono tutaendelea, pamoja tutaenda mbali World Vision itaendelea kufanya kazi, mmejengewa uwezo msimame imara” alisema Gambo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mradi wa Kizazi Kipya, Pendo Mwaisese alisema kuwa mradi wa Kizazi Kipya umejikita kwenye vipaumbele vinne. Alivitaja vipaombele hivyo kuwa ni afya, elimu, kuinua vipato vya kaya pamoja na ulinzi na usalama. Mradi huo umewanufaisha vijana waliotoka katika mazingira magumu kwa kuwapatia ujuzi wa kufanya kazi, watoto kutoka kaya maskini wamenufaika kwa kupelekwa shule na kupatiwa mahitaji ya kielimu, alisema.
Akitoa ushuhuda wa namna alivyonufaika na mradi wa kizazi kipya, mnufaika Frank Mlewa alisema kuwa mradi huo umemsaidia kupata ujuzi wa ufundi kwa sababu alipelekwa kusoma ufundi katika chuo cha VETA. “Mradi umenikuta nikiwa mtaani, tulikuwa wengi ulitukusanya ukatuunganisha pamoja ukatupa elimu katika chuo cha ufundi na sasa ni fundi. Naweza kujitegemea na nimepanga kwa sasa najitegemea” alisema Mlewa.
Mradi wa Kizazi Kipya ulianza mwaka 2016 umehudumia jumla ya vijana na watoto 1,472 na unatarajiwa kuisha Septemba 2021 ukisimamiwa na kutekelezwa na mashirika ya Action for Community Care (ACC) na KISEDET ambayo yanapokea fedha kutoka Pact Tanzania.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.