NAIBU Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde amewataka wadau wote wa maendeleo ambao wanatekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuvutia na kuinua vijana katika sekta ya kilimo kufuata muelekeo wa Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Building a Better Tommorow - BBT) ili kuongeza wigo mpana zaidi wa kuwafikia vijana wengi.
Wito huo umetolewa Jijini Iringa na Naibu Waziri Mavunde aliposhiriki katika uzinduzi wa Mradi wa kuwawezesha Vijana na Wanawake katika mnyororo wa thamani wa kilimo awamu ya pili (Generation Food Accelerator II) chini ya ufadhili wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kupitia mradi wa Agri-connect.
"Ni dhahiri kwamba ninyi wadau, mkishirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi yenu, kutaleta tija kubwa zaidi kutokana na kwamba, kutazuia upelekaji wa rasilimali fedha katika eneo hilo hilo moja kwa Serikali na wadau wa sekta binafsi.
Changamoto zinazowakabili vijana katika kilimo zinafahamika zikiwemo ukosefu wa ardhi, mitaji, pembejeo, miundombinu ya umwagiliaji na uhifadhi na masoko ya uhakika ya mazao watakayozalisha.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya utashi wa kisiasa na mkazo mkubwa kwenye kilimo aliyouweka Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inakwenda kutatua changamoto hizo kupitia programu ya vijana ya _*Building a Better Tommorow *_kwa kuwatafutia ardhi na kuwamilikisha, kujenga miundombinu ya umwagiliaji na uhifadhi, kuwapatia pembejeo, kuwapa mitaji na kuwaunganisha na masoko ya uhakika.
Tunataka na ninyi wadau wote wa maendeleo ya masuala ya vijana kuhakikisha kwamba katika utekelezaji wa programu zenu mbalimbali mnazingatia mipango na muelekeo wa serikali katika kuwahudumia vijana kwenye sekta ya kilimo.
Nimefurahishwa na namna ambavyo mradi huo umepangwa kutekelezwa ambapo kiasi kikubwa cha fedha kitaelekezwa katika kuwapa vijana mitaji na ujenzi wa miundombinu, hali aliyoeleza kuwa uendelevu mkubwa kwa kijana hata pale ambapo mradi utafika mwisho,” alisema Mavunde
Awali, akitoa wasilisho, Mratibu wa mradi huo Ronald Mtana alieleza kuwa mradi huo ambao utawafikia vijana 30,000 wenye thamani ya Shilingi milioni 726 utatekelezwa kwa awamu katika Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Katavi.
Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Uzalishaji Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Beatrice Banzi alieleza umuhimu wa sekta binafsi kuchangia jitihada za Serikali kutatua changamoto za vijana na kutoa wito kwa wadau wote wenye utayari kujiunga katika utekelezaji wa programu ya kuwezesha vijana kushiriki kilimo chenye tija.
Akitoa salamu zake, Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la RIKOLTO ambao ni sehemu ya watekelezaji wa mradi huo, Kein Mvanda aliishukuru Serikali kwa kuja na mradi wa BBT na kuahidi kuwa RIKOLTO itaendelea kutekeleza miradi na mipango yake kwa vijana kwa kufuata muelekeo na vipaumbele vya Serikali kupitia programu ya BBT.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.