Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo ameutaka uongozi wa kituo cha Afya Makole kilichopo manispaa ya Dodoma kuendelea kujizatiti katika matumizi ya mfumo wa uendeshaji na usimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya - GoTHoMIS ili kuboresha utoaji wa huduma na kudhibiti ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Mhe. Jafo ameyasema hayo wakati alipotembelea kituo cha Afya Makole kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Serikali yaliyoelekeza ufungaji wa mifumo ya kielektroniki katika vituo vya kutolea huduma za Afya ili kuweka kumbukumbu ya taarifa zote za wagonjwa na sambamba na taarifa za fedha zinazotolewa na wagonjwa kuchangia huduma za Afya.
Mhe. Jafo amesema ameridhishwa na ufungaji na matumizi ya mfumo wa GoTHoMIS ambao kwa kiasi kikubwa unasaidia utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa na zaidi ya hapo kutunza taarifa zote za wagonjwa lakini mfumo huu haujatumika vizuri katika eneo la mapokezi ya fedha za uchangiaji wa huduma za Afya kwa sababu mapato ya kituo cha Makole hayajaongezeka kadiri inavyotakiwa.
Aliongeza kuwa "Mfumo huu ni mzuri sana katika uendeshaji na usimamaizi wa shughuli zinazotolewa katika vituo vya huduma za Afya, lakini sijaridhishwa na namna ambavyo mnautumia katika ukusanyaji wa mapato ya kituo cha Afya Makole".
Ninauhakika mfumo huu hamjautumia ipasavyo, haiwezekani mkakusanya shilingi milioni 9 kwa mwezi ingawa mapato yameongezeka kutoka shilingi milioni 3 mlizokuwa mnakusanya hapo awali ila ninauhakika mnaweza kukusanya zaidi ya kiasi hiki, hii ni kutokana na ukubwa wa kituo na idadi ya wagonjwa wanaotibiwa kwa siku.
Aliongeza kuwa "Kuwepo kwa mifumo ni jambo moja na kuutumia ipasavyo ni jambo lingine, jambo la msingi hapa ni uaminifu katika matumizi ya mifumo hii, kuna watu katika katika vituo hivi uaminifu ni mdogo hivyo husababisha kutoelewana baina ya wafanyakazi kwa kuwa sio wote wanaonufaika na udanganyifu huo lakini pia ni hasara kwa taifa".
Mhe. Jafo amewataka watumishi wa Makole kuongeza jitihada katika kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali na kuongeza uaminifu katika kila eneo linalohusu fedha za umma. Pia amewataka wataalam wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa weledi na kutoa huduma stahiki kwa watumiaji wa kituo hicho na kuwataka kufuatilia fedha zilizotolewa na Serikali takribani milioni 500 kwa ajili ya ujenzi ya ukarabati kuhakikisha zinatumia pesa hizo kwa mujibu wa makubaliano katika uboreshaji wa vituo hivyo mpaka ifikapo 30 Disemba 2017.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.