NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake Jinsia na Makundi Maalum Mhe. Mwananidi Ali Khamis ameipongeza Taasisi ya Jamiiiyaatul Akhlaaqul Islam (JAI) kwa mchango wake katika kusaidia wanawake na watoto wenye mahitaji maalum.
Naibu Waziri Mwananidi amesema hayo Januari 04, 2025 wakati wa tamasha lilioandaliwa na Taasisi hiyo kwa ajili ya harambee ya kuchangisha fedha ili kununua nyumba itakayokuwa kituo maalum cha kuratibu utoaji wa huduma na mahitaji kwa Watu Wenye Uhitaji hasa walio katika hospitali za Mkoa wa Dar es Salaam hususani Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Amesema kwamba Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara za Kisekta, Taasisi na Mamlaka za Umma zinaendelea kushirikiana na Viongozi wa Taasisi za Dini wakati wa kuandaa bajeti na kutekeleza afua zinazolenga kuimarisha Ustawi na Maendeleo ya jamii nchini.
"Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inathamini na kutambua mchango unaotolewa na Taasisi za Dini kwa lengo la kudumisha amani, kuimarisha umoja wa kitaifa pamoja na kutoa huduma katika jamii kwa lengo la kuboresha maisha ya mtu mmoja na taifa kwa ujumla" amesema Naibu Waziri Mwanaidi
Aidha Naibu Waziri Mwananidi amesizitiza wafanyabiashara ndogondogo kutoka makundi ya Wanawake, Vijana, Watu Wenye Ulemavu kote nchini kufika Halmashauri za Wilaya hususan katika Ofisi za Maendeleo ya Jamii ili kupewa utaratibu wa kujiandikisha na kujisajili kwa lengo la kupata vitambulisho vya kidijitali vya Wafanyabiashara Wadogo ambavyo vitawasaidia kupata mkopo inayotolewa na Serikali kupitia Benki ya NMB na Taasisi zingine za kifedha.