NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Josephat Kandege amesema amefurahishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea katika Jiji la Dodoma.
Kandege ameyasema hayo alipofanya ziara yake katika Miradi mitatu mikubwa ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jiji la Dodoma.
Miradi ambayo imetembelewa na Naibu Waziri huyo ni pamoja na Ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi, Kituo kikubwa cha kisasa chenye uwezo wa kuingiza Mabasi 250 na kuhudumia abiria zaidi ya 6,000 kwa wakati mmoja.
Naibu Waziri huyo pia, alitembelea Ujenzi wa Soko la kisasa pamoja na Kituo cha Mapumziko cha Chinangali, ambapo miradi yote hii inatekelezwa na Mkandarasi Mohammedi Builders Limited na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi wa tisa mwaka huu.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Josephat Kandege (katikati) akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi (Wa pili kushoto) juu ya hatua iliyofikiwa kwenye Ujenzi wa Soko kuu la kisasa.
“Sura ya Tanzania kwa sasa ni Dodoma kwa hiyo tusingependa miradi hii ichelewe kukamilika, tunapenda ikamilike kwa wakati, nitafurahi kama mtafanya hivyo kwa sababu bado Mkandarasi una muda wa kutosha kukamilisha miradi hii” Alisema Mhe. Kandege.
Naibu Waziri Kandege alisema kuwa lengo Kuu la ziara yake hiyo ni kujiridhisha na utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
Hata hivyo, ameridhishwa na namna miradi hiyo inavyotekelezwa kwa uwazi na kumpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi kwa jinsi anavyosimamia vizuri mapato na matumizi ya fedha za miradi hiyo.
“Serikali imeweka nguvu kubwa katika kuhakikisha miradi mikubwa kama hii inatekelezwa, hivyo nitumie fursa hii kukupongeza Mkurugenzi kwa namna unavyotekeleza na kusimamia miradi hii kwa ukaribu mkubwa” Alisema Mhe. Kandege.
Aidha, akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alimshukuru Mhe. Kandege kwa kufanya ziara hiyo na kumhakikishia kuwa miradi hiyo itakamilika kwa ubora unaotakiwa na kwa wakati.
“Mhe. Naibu Waziri kwanza nikushukuru kwa kututembelea kwa lengo la kuona hatua ambayo tumefikia katika miradi hii, Ofisi yangu imejipanga vizuri katika kufuatilia maendeleo ya miradi hii na kuhakikisha inakamilika kwa wakati” Alisema Kunambi.
Naibu Waziri Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Josephat Kandege (Kushoto) akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi pamoja na Mkandarasi, kuhakikisha Ujenzi wa Soko kuu la Kisasa unakamilika kwa wakati.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.