WATUMISHI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kupanda miti 10 kila wiki ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya kukijanisha Dodoma na kulifanya Jiji la Dodoma kuwa na hali nzuri ya hewa na mazingira.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge baada ya kuongoza zoezi la upandaji miti katika eneo la Medeli jijini humo leo.
Dkt. Mahenge aliagiza kuwa, kila mtumishi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma apande miti 10 kwa wiki. “Nataka kila mtumishi kuanzia leo, kila wiki lazima apande miti 10. Miti hiyo nataka iwekewe alama au jina lake ili iwe rahisi kutambulika” alisema Dkt. Mahenge.
Katika kulifanya zoezi hilo kuwa na umuhimu alishauri kuwa watumishi wanaweza kushirikisha familia au marafiki zao katika kupanda miti hiyo na kwamba utekelezaji wa zoezi hilo utakaguliwa na kuingizwa katika taratibu za kiutumishi ili iwe rahisi kuchukua hatua stahiki kwa mtumishi atakayeshindwa kutekeleza.
Mkuu huyo wa Mkoa alikemea tabia ya baadhi ya watu kudharau zoezi la upandaji miti na utunzaji wa mazingira jijini hapa. “Kuna baadhi ya watu wanadhani mabadiliko ya kuifanya Dodoma ibadilike na kuwa ya kijani ni la watu wengine. Dhana hiyo siyo sahihi, jukumu hili ni letu sote, watu wanasubiri mazingira yatengenezwe na kuwa mazuri kisha waje kufanyia sherehe. Upandaji miti na utunzaji mazingira ni wajibu siyo ‘ceremonial" alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Akisoma taarifa fupi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka ngumu, Dickson Kimaro alisema kuwa, katika kufanikisha kampeni ya kijanisha Dodoma ifanikiwe ni jukumu la kila mwana Dodoma na wadau kupanda miti kwenye maeneo mbalimbali kwa lengo la kuboresha Mazingira ya Dodoma.
“Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha lengo ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani linafanikiwa. Jitihada hizo ni pamoja na utengaji na uainishaji wa maeneo mahsusi kwa ajili ya kupanda miti, uendelezaji wa bustani za kuzalisha miche, utoaji wa elimu kwa umma kuhusu Dodoma ya kijani pamoja na kuweka Mazingira wezeshi kwa wadau mbalimbali wenye nia ya kuunga mkono na kuendeleza jitihada za Serikali za kuifanya Dodoma kuwa ya kijani” alisema Kimaro.
Akiongelea mikakati ya Halmashauri katika kukijanisha Dodoma, aliitaja kuwa ni kuhakikisha kila mwananchi anashiriki katika upandaji miti ambapo kila mkazi wa Dodoma anatakiwa kupanda miti angalau mitano katika eneo lake ikienda sambamba na kudhibiti ukataji miti ovyo bila ya kibali cha Afisa Mwidhinishaji kutoka Jiji.
Mikakati mingine aliitaja kuwa ni “Sheria ndogo za utunzaji na usimamizi wa Mazingira za Jiji la Dodoma zimesambazwa katika Kata na Mitaa ili kudhibiti mifugo inayokula miti iliyopandwa na uvamizi wa jamii kwenye misitu ya asili. Pia kutoa elimu ya upandaji miti kulingana na majira ya mvua katika Kata 41 za Halmashauri ya Jiji na kuhamasisha upandaji miti kuanzia kwenye ngazi ya kaya, taasisi na uanzishwaji wa mashamba ya miti kwa mitaa yenye maeneo makubwa kwa njia ya matangazo ya barabarani” alisema Kimaro.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema Halmashauri hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 2,576 itaendelea kushirikisha wadau mbalimbali katika utekelezaji wa kampeni ya kijanisha Dodoma huku akimshukuru Mkuu wa Mkoa huo, Mkuu wa Wilaya, na wadau wote waliojitokeza kwa wingi katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Katika zoezi hilo la upandaji miti lililoongozwa na Mkuu wa Mkoa, lilihudhuriwa na wakuu wa taasisi mbalimbali, wanafunzi kutoka vyuo vikuu na wananchi, jumla ya miti 2,140 ilipandwa.
Kampenzi ya kijanisha Dodoma ilizinduliwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan Disemba 21, 2017 kwa kupanda miti katika bonde la chanzo cha maji cha Mzakwe Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru akipanda mti katika zoezi lililoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Binilith Mahenge
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Biilith Mahenge (wa kwanza kulia) akimsikiliza kwa makini Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma alipokuwa akielezea kuhusu utekelezaji wa zoezi la kupanda miti Jijini Dodoma pamoja na mikakati kuhakikisha kuwa zoezi la upandaji miti linakukwa endelevu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.