RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan amesema kuwa nchi ipo salama na ataendeleza yale ambayo aliyekuwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alitamani kuyafikisha kwa maslahi ya watanzania.
Rais, Mama Hassan amesema hayo leo alipokuwa akitoa salamu katika uwanja wa Jamhuri jijini hapa katika zoezi la kitaifa la kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Mafuguli.
Rais, Mama Hassan amesema “Nchi yetu ipo katika mikono salama, mimi na mwenzangu Rais, wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi tutaendeleza na tutafika pale alipotamani Hayati Dkt. John Pombe Magufuli”.
“Katika uongozi wake tumejifunza vizuri, tumepikwa vizuri na tumeiva sawasawa. Tupo tayari kuendeleza kazi yake nzuri kwa nguvu, kasi na ari ile ile. Kwa wale ambao wanamashaka, mwanamke huyu ataweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nataka niwaambie kwamba aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye maumbile yake ni mwanamke” amesema Rais huyo kwa kujiamini.
Akiongelea mahusiano ya Tanzania na nchi jirani, Rais huyo amesema uwa mahusiano hayo yataendelea kuwa imara na kuimarika zaidi chini ya uongozi wake.
Akimuongelea mwenda zake Hayati Dkt. Magufuli, amesema kuwa katika kipindi cha miaka sita ya utawala wake alijenga uchumi wa ndani unaotegemea mapato ya ndani, akiwekeza katika ujenzi wa miradi ya kimkakati. “Rais, Dkt. Magufuli alidhamiria kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii kama afya na elimu. Kutokana na dhamira hiyo, leo watanzania wengi wanyonge na masikini wanamlilia” amesema Rais Mama Hassan.
Hofu yake kwa Mungu ndiyo iliyomfanya kuwa na mapenzi makubwa kwa wanyonge na masikini wa Tanzania, hakuwahi kukosa muda wa kusali na kuabudu, aliongeza na kuwataka watanzania kutumia kipindi hicho cha maombolezo kumshukuru Mungu.
Rais Mama Hassan amesema kuwa Hayati Dkt. Magufuli hakuogopa kutetea alichoamini kuwa ni sahihi kwa maslahi ya Taifa hata kama kinahatarisha maisha yake. “Umati huu uliojitokeza na simanzi kubwa ni kielelezo tosha cha pigo kwa watanzania” amesema Rais, Mama Hassan.
Akiongelea imani ya Hayati Dkt. Magufuli kwake, amesema kuwa daima atamshukuru kwa imani kubwa aliyoiweka kwake na kwa wanawake wote wa Tanzania. “Tukiandika historia ya usawa, jina lake litakuwepo, kupitia yeye Tanzania ilipata nafasi ya mwanamke wa kwanza Makamu wa Rais na sasa Rais. Hii inanipa faraja kwa miaka sita nilihudumu kama msaidizi wake wa kwanza na wa karibu” amesema Rais, Mama Hassan.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi amesema kifo cha Hayati Dkt. Magufuli kimetingisha bara zima la Afrika. “Msiba huu siyo tu, unawagusa watanzania peke yao, kuondoka kwa Dkt. Magufuli kumetingisha bara zima la Afrika. Bara la Afrika linajikuta katika taharuki ya kupoteza mwanasiasa aliyekuwa anaboresha maisha ya wananchi wake na aliyelenga kutetea na kuboresha uchumi wa kijamii katika bara la Afrika” amesema Rais, Tshisekedi.
Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Afrika, amesema kuwa watabaki na kumbukumbu ya Hayati Dkt. Magufuli kama mpiganaji, mzalendo, siyo tu kwa maslahi mapana ya Tanzania bali kwa Umoja wa Afrika.
Zoezi la kitaifa la kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania limefanyika Kitaifa katika uwanja wa Jamhuri na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa Nchi tisa na viongozi wengine wa mashirika ya kimataifa na Mabalozi mbalimbali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.