NDEGE kubwa aina ya Airbus A220-300 yenye uwezo wa kubeba abiria 132 na kutumia muda wa dakika 45 kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam, imetua kwa mara ya kwanza katika uwanja wa ndege wa Dodoma baada ya uwanja huo kufanyiwa marekebisho makubwa kwa kuongezwa njia ya kutua na kurukia ndege kufikia urefu wa kilometa 2.8.
Ndege hiyo 'Ngorongoro Hapa Kazi' ilitua leo majira ya saa 10:43 jioni na kupokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Leonard Chamurilo.
Akielezea zaidi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale amesema "Serikali iliamua kuongeza uwezo wa uwanja huo ili kuwe na ufanisi katika kuziendesha ndege zetu, kazi hii tulianza Julai 2020 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 3.506"
Aidha, alisema kazi hiyo ilihusisha ujenzi wa eneo la maegesho ya ndege hiyo. Kulilipwa fidia ya shilingi bilioni 5.8 kwa watu ili kupisha ujenzi huo na kazi iliyobaki ni kuweka taa ili kuruhusu ndege hiyo kutua hata usiku.
Akishiriki katika mapokezi hayo ya kihistoria kwa Jiji la Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kufanikisha ununuzi wa ndege na kuboresha wigo wa usafiri wa anga hadi kufikia Dodoma. Amesema hii ni fursa kwa watu wa Dodoma na duniani kote kwa kuwa fursa za urahisi wa usafiri na uwekezaji zinazidi kuongezeka Jijini Dodoma.
'Hii ni katika kuanza utekelezaji wa mpango wetu wa kibiashara, tuna kituo kikuu Dar es Salaam, na tuna vituo vya kuunganisha ikiwepo Dodoma, Zanzibar, Kilimanjaro, Mwanza na Mbeya. Hivyo ni vituo ambavyo tutaendelea kuongeza taratibu safari zetu za ndege kuunganisha na mikoa mingine na baadae na nchi za nje". Amesema Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi.
Naye Mkurugenzi Mkuu Mamlaka Usafiri wa Anga Hamza Johari amesema kuwa uwanja wa Dodoma ulikuwa na uwezo wa kuruhusu kutua ndege yenye uwezo wa Q400 ambayo inabeba abiria 76, baada ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais na kwa kuwa Dodoma sasa imeshakuwa Makao Makuu, kazi ilifanyika ya kuongeza urefu wa barabara na kutengeneza taratibu za anga ambazo zinaiwesha ndege kubwa kama hii kutua na kuruka hapa chini salama ni mifumo inayotumia satelaiti.
Akimalizia Mkurugenzi huyo amewashukuru wadau wote kuanzia TANROADS, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Mamlaka ya viwanja vya usafiri wa anga pamoja na Wizara yetu na Mheshimiwa Rais kwa mwongozo wake uliowawezesha kufanya kazi hiyo kwa haraka na ndege kubwa inaweza kutua.
Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi akitoa maelezo kuhusu ndege aina ya Airbus aliyotua Jijini Dodoma kwa mara ya kwanza.
Abiria waliokuwa kwenye ndege hiyo wakishuka huku wakishuhudiwa na viongozi na baadhi ya wakazi wa Jiji la Dodoma.
Ndege hiyo Airbus A220-300 ikimwagiwa maji na magari ya Zimamoto kama ishara ya kuikaribisha.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.