NDEGE kubwa aina ya Airbus (200-300) zinazobeba abiria hadi 132 zitaanza kutua rasmi katika Kiwanja wa Ndege Dodoma Oktoba Mosi mwaka huu baada ya ujenzi na urefushaji wa barabara za kurukia ndege kukamilika.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mhandisi wa Tanroads Mkoa wa Dodoma, Salome Kaganda wakati akitoa taarifa fupi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge aliyetembelea uwanja huo jana. Awali uwanjani hapo zilikuwa zikitua ndege za ukubwa wa kati kama Bombardier Dash 8 Q400 zikitoa huduma kwa abiria 76-78, sasa zitaanza kutua ndege kubwa hadi aina ya Airbus.
Akizungumza uwanjani hapo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge alisema hayo ni mabadiliko makubwa yaliyofanyika tangu Serikali ya Rais John Magufuli kuhamia jijini Dodoma.
Dkt. Mahenge alisema ujenzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma umetumia zaidi ya Sh. Bilioni 25 na utakabidhiwa rasmi kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) Oktoba Mosi mwaka huu na ndege kubwa zitaanza kutua rasmi.
Akitoa maelezo, Mhandisi Kaganda alisema, ujenzi na urefushaji wa uwanja huo utakamilika katika kipindi cha wiki mbili zilizobaki kama mkataba unavyoonesha. Ujenzi huo ulianza Juni 2016, na ulihusisha ujenzi wa barabara ya kurukia ndege yenye urefu wa mita 2,500 na upana mita 30, barabara za viungio, maeneo ya kuegesha ndege na taa za kuongozea ndege nyakati za usiku.
“Mradi wa ujenzi huo unatekelezwa na kampuni ya M/S China Henan International Cooperation Limited (Chico) kwa gharama ya Sh. Bilioni 11 kwa miezi sita na kusimamiwa na wahandisi wa Tanroads na Taa),” alisema.
Ujenzi au urefushaji unaoendelea sasa unahusisha urefushaji wa barabara ya kurukia ndege kwa mita 250 na upana mita 30 eneo la kugeuzia ndege, eneo la kuegeshea ndege lenye urefu wa mita 80 na upana meta 70 na urefushaji uzio wa usalama kwa gharama ya Sh bilioni 3.5.
Pia ujenzi na ukarabati huo ulioanza Juni 2016 ulihuisha ulipaji fidia Sh bilioni 11.4 kwa wananchi 168 ambao waliathirika na upanuzi na urefushaji wa uwanja huo mita 550 na upana mita 150.
Hivyo urefushaji wa barabara za kurukia ndege kutoka mita 2,500 za sasa hadi mita 2,750 utawezesha ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba abiria hadi 132 (airbus 220-300) kutua katika Kiwanja cha ndege cha Dodoma na hivyo kurahisisha huduma za usafiri katika Jiji la makao makuu ya nchi.
Akizungumza Meneja wa Uwanja wa Ndege (TAA) Dodoma, Bertha Bankwa alisema kutokana na ukarabati huo, uwanja huo utakuwa na uwezo wa kutua ndege kubwa, alisema awali uwanja huo zilikuwa zikitua ndege ndogo lakini ukarabati ukikamilika basi zitakuwa zikitua ndege kubwa usiku na mchana kazi yote imefikia asilimia 70.
Bankwa aliongeza kuwa, pamoja na kukamilika uwanja huo, bado kutakuwa na changamoto chache zikiwemo za majengo marefu karibu na uwanja pamoja na nyumba nne zilizo karibu na eneo la kugeuzia ndege mambo ambayo yanatafutiwa ufumbuzi chini ya uongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCCA) pamoja na taasisi mwambata jijini kuzungumzia changamoto hizo.
Taasisi zitakazokutana hivi karibuni kutafuta suluhisho kuhusu kuongeza eneo la kugeuzia ndege pamoja na majengo marefu karibu na uwanja ni pamoja na TAA, Wakala wa Barabara Mjini (Tanroads), Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na taasisi nyingine.
Mkuu wa Mkoa Dkt. Mahenge alisema, atawasiliana na taaasisi hizo zinazokutana ili kuhakikisha zinatatua changamoto hizo ili ikifika Oktoba mosi ndege kubwa zianze kutua.
Meneja wa Uwanja wa Ndege (TAA) Dodoma, Bertha Bankwa akitoa maelezo kuhusiana na ujenzi wa kiwanja wa ndege Jijini Dodoma na faida za ujenzi huo baada ya kukamilika.
Moja ya maeneo ambayo yameongeza ukubwa na urefu wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.