SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai ameomba Serikali kuboresha sheria ya uwezeshaji kwa wanafunzi katika ngazi zote na sio kutoa kipaumbele kwa Elimu ya juu pekee.
Spika Ndugai ambaye ni Mkuu wa Mhimili wa Bunge alisema hayo jana Mei 11, 2021 katika kilele cha mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) kwa mwaka 2021, yaliyofanyika Jijini Dodoma katika uwanja wa Jamhuri.
“Tunaiomba Serikali iangalie ule mfumo unaowasaidia wanafunzi wa Elimu ya juu, ile sheria tuiangalie upya kwa pamoja Serikali na Bunge, ili badala ya kuangalia wanafunzi wa Elimu ya juu peke yake, tuweze kuangalia na jinsi ya kuwasaidia wanafunzi wa vyuo vya kati” alisema Spika Ndugai.
Spika Ndugai aliongeza kuwa Serikali inapaswa kuangalia taasisi zetu za utafiti kwa ukarimu kwa sababu ndiyo matokeo ya tafiti mbalimbali yanaweza kutusogeza mbele kiuchumi na kutusaidia kwenye sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda.
Spika Ndugai alionyesha kuvutiwa na mashindano hayo yaliyofanyika kwa mara ya tatu mfululizo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambapo aliwakaribisha Wizara husika kuendelea kuandaa mashindano hayo ndani ya jiji hilo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge alisema kuwa Dodoma inasifa zote za kuendelea kupata kipaumbele katika mashindano hayo na anawakaribisha watu wote pia wawekezaji Mkoani hapa.
Aidha, Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga alieleza kuwa, mashindano hayo yalianzishwa mwaka 2019, ikiwa ni moja ya mikakati ya Wizara ya kuibua, kutambua na kuendeleza ubunifu na ugunduzi unaofanywa na Watanzania ususani wa ngazi ya chini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.