Na. Sifa Stanley, DODOMA
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru ametangaza neema ya kuhamishwa wafanya biashara ndogondogo kutoka maeneo ambayo siyo rasmi na kuwapanga katika Soko la Wazi la Machinga kwa amani na utulivu ili waendelee kutekeleza majukumu yao.
Neema hiyo ameitangaza leo katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ambapo Mkurugenzi huyo aliongea na waandishi wa habari kuhusu kukamilika kwa Soko la Wazi la Machinga na kuwaeleza kuwa Machinga watahamishwa na kuingia sokoni kwa njia ya amani na hakuna vurugu yoyote itakayotokea.
Mkurugenzi Mafuru alisema “kuanzia leo tarehe 07/09/2022 mpaka tarehe 23/09/2022 wafanyabiashara wote niliowataja wanatakiwa wawepo ndani ya soko lile. Tumeshakubaliana Dodoma toka mwanzo kuwa hatapigwa mtu kirungu wala hatasukumwa mtu”.
Akizungumzia namna Jiji la Dodoma litakavyonufaika na ujenzi wa soko hilo, Mafuru alisema kuwa, kukamilika kwa Soko la wazi la Machinga kutasaidia jiji la Dodoma kuwa safi, na kutachangia mapato makubwa kwa Halmashauri.
“Huu mradi unakwenda kufanya mapinduzi kwa Jiji la Dodoma, cha kwanza tunachokwenda kukipata katika mradi huu, Jiji la Dodoma linakwenda kuwa safi katika kiwango hakijawahi kutokea tangu Dodoma kuumbwa. Tulichogundua na hata viongozi wa juu wamegundua hilo wafanyabiashara ndogondogo walifanya mji uonekane haupendezi pia soko hili litachangia mapato ya shilingi bilioni 1.2 ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka” alisema Mafuru.
Aidha, akieleza uwezo wa soko ni kubeba wafanyabiashara 5,000. Akiongelea bidhaa zinazopatikana sokoni hapo alizitaja kuwa ni vitabu na shajara, nguo na viatu, vifaa vya umeme. Nyingine alizitaja kuwa ni vifaa vya nyumbani pamoja na huduma ya saluni za kike na kiume.
Ujenzi wa Soko la wazi la Machinga umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 9.53, na ulianza rasmi mwaka 2021 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyeagiza Machinga wote nchini wapangwe katika maeneo rasmi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.