SHIRIKA la Nyumba nchini (NHC) linakusudia kujenga nyumba 1,000 mkoani Dodoma za kuuza na kupangisha kwa lengo la kutumia fursa ya Serikali kuhamia mkoani hapo.
Akizungumza jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Maulid Banyani mbele ya Kamati ya Hesabu za Serikali alisema hivi sasa wapo kwenye mazungumzo na watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kujenga nyumba hizo jijini hapo. Alisema mazungumzo yakikamilika yatalifanya shirika hilo kujenga nyumba hizo kwa ajili ya kupangisha na kuuza kwa watumishi na watu mbalimbali waliopo makao makuu ya serikali.
Mkurugenzi Mkuu alitoa ufafanuzi huo kutoka kwa Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbaruku aliyetaka kujua NHC imejipanga vipi kulitumia soko la Dodoma kwa kujenga nyumba za kupangisha na kuuza. Banyani alisema kutokana na serikali kuhamia Dodoma, shirika hilo limejipanga kutumia fursa hiyo kwa kujenga nyumba nyingi za kuuza na kupangisha wafanyakazi wengi wa serikali waliohamia jijini hapo.
Ili nyumba hizo zipangishwe au kuuzwa kwa bei nafuu, Banyani alisema mazungumzo bado yanaendelea kufanyika na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango ili kupatikana kwa mkopo wa nyumba ili zijengwe kwa bei nafuu na zipangishwe kwa bei nafuu. Alisema mazungumzo hayo yanahusisha serikali kupitia Benki Kuu na Benki ya Dunia kupitia Benki ya Afrika yakikamilika na kufikia makubaliano ya kukopa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kutasaidia nyumba hizo kupangishwa kwa bei nafuu na kugusa watu wa kipato cha chini.
“Mkopo huo kwa ajili ya ujenzi utasaidia kupunguza bei ya nyumba hizo ambazo zinajengwa kwa lengo la kuwasaidia watu wa kipato cha chini,” alisema.
“Kwa kupitia mikopo ya nyumba utasaidia wateja wa nyumba hizo kununua kwa bei ya punguzo la asilimia 11 na hivyo kusaidia watu wa kipato cha chini kununua nyumba hizo,” alisema.
Lakini pia ili kuhakikisha NHC inatumia gharama ndogo za ujenzi nyumba hizo, inakusudia kupunguza gharama za kujenga majengo hayo kwa kutumia makandarasi wake wa shirika hilo.
Chanzo:Tovuti ya HabariLeo
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.