Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amepiga marufuku shule zote nchini kuwapa wasichana dawa aina ya Folic Acid na badala yake shule zimetakiwa kuwajengea uwezo wa kulima maboga na mbogamboga katika bustani zao.
Waziri Ummy amesema hayo jana (8/8/2020) wakati alipokua akihitimisha kilele cha Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki inayojumuisha Mikoa ya Dar Es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro ambayo yamefanyika mkoani Morogoro.
Mhe. Ummy amesema kuwa ni marufuku kuwapa wanafunzi na wasichana balehe vidonge vya Folic Acid, badala yake fedha hizo zinazotolewa kwa ajili ya dawa hizo zitumike kuanzisha bustani shuleni ili kuzalisha vyakula vinavyotoa madini hayo.
“Mbali na kuanzishwa kwa bustani shuleni lakini pia fedha hizo zinaweza kupelekwa kwa vijana ili waanzishe miradi ya bustani za mboga kwa ajili ya kuzalisha mazao yanayozalisha asidi hiyo yakiwemo maboga, matunda na hata karoti badala ya kutoa vidonge kwa wanafunzi”. Amesema Ummy.
Kuhusu unywaji wa maziwa mashuleni, Waziri Ummy amesema kuwa atamwandikia barua ya pendekezo Waziri wa Elimu Prof. Joyce Ndalichako ili kuanzia Septemba mosi mwaka huu kila shule iwe na kibanda cha maziwa kwa ajili ya wanafunzi kununua.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaonesha kwamba kila mtu anatakiwa kunywa nusu lita ya maziwa sawa na lita 180 kwa mwaka, lakini kwa sasa kila mtu anakunywa lita 40 kwa mwaka sawa na vijiko 10 vya chai kwa siku.
Pia Waziri amesema udumavu kwa watoto wa chini ya miaka mitano umepungua nchini kutoka asilimia 34.4 mwaka 2014 hadi asilimia 31.8 mwaka 2018 licha ya kuwa jitihada zinatakiwa kuendelea kuchukuliwa.
Pamoja na hayo Waziri huyo ameupongeza mkoa wa Morogoro kwa kuwa mwenyeji wa maonesho hayo ambayo yamekuwa chachu ya ukuaji wa kilimo, uvuvi na ufugaji pamoja na ujasiriamali nchini na amewataka waratibu wake kutoishia hapo na badala yake ujuzi huo upelekwe vijijini kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo muhimu ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia pato la taifa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.