Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kudumisha nidhamu, uadilifu na uhusiano mahali pa kazi ili kuleta ufanisi mzuri wa kazi kati yao na wanao waongoza.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu mpya wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Mhe. Josephat Maganga alipofanya kikao cha kujitambulisha kwa Mkurugenzi na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri hiyo.
Maganga amesema kuwa uadilifu na nidhamu ni vitu vya msingi katika kazi kwani vinaleta ufanisi mkubwa kwa viongozi na wale wanaowaongoza huku akiwaasa kuepuka kusababisha mikwaruzo baina yao kwani vitu hivyo vinaweza kudidimiza uchumi wa Halmashauri na kuleta matokeo mabaya hasa kwenye ukusanyaji wa Mapato.
“Tuepuke kujiona mimi ni mkubwa kuliko yule, hizi nafasi zetu ni za kupita tu, mtu anaweza akakusoea huko mtaani kwenye mambo yenu binafsi, hiyo isikufanye wewe kutompatia haki yake mahali mnapofanyia kazi.” Alisema Maganga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Godwin Kunambi amemkaribisha Dodoma Mkuu huyo wa Wilaya na kumpongeza kwa uteuzi wake huku akimhakikishia ushirikiano kati ya Halmashauri na Ofisi yake kama ilivyokua kwa Mkuu wa Wilaya aliyepita.
“Mkuu wa Wilaya, mafanikio yote unayoyaona hapa Jijini yamesababishwa na hawa Wakuu wa Idara na Vitengo katika Halmashauri hii, tumekuwa tukishirikiana, tukifanya kazi mchana na usiku kuhakikisha Jiji letu linakua la mfano, kwa hiyo nikuhakikishie kuwa tutashirikiana ipasavyo na Ofisi yako ili kuleta maendeleo zaidi.” Alizungumza Kunambi.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Josephat Maganga akisisitiza jambo kwa Timu ya Menejimenti ya Jiji la Dodoma alipofanya ziara ya kujitambulisha katika taasisi hiyo iliyo katika Wilaya yake.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Mhe. Josephat Maganga (katikati) akipokea moja ya vitabu vyenye taarifa za utatuzi wa migogoro katika Jiji la Dodoma kutoka kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi. Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma Mjini Michael Maganga.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Josephat Maganga (aliyesimama) akiongea na timu ya menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma (baadhi wanaonekana pichani) wakati alipotembelea ofisi za Jiji kujitambulisha.
Baadhi ya wajumbe wa Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya JIji la Dodoma wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini (hayupo pichani) alipokuwa akionea nao leo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.