Na. Leah Mabalwe, KIKUYU KASKAZINI
Kampeni ya kuhakikisha jamii inabaki salama na utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati safi katika Kata ya Kikuyu Kaskazini, imeongeza tija na uelewa kwa taasisi za elimu kuhamia katika matumizi ya nishati safi.
Hayo yalielezwa na Diwani wa Kata ya Kikuyu Kaskazini, Israel Mwansasu mbele ya waandishi wa habari waliotembelea kata yake kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka minne.
Alisema kuwa nishati safi ni jambo muhimu sana katika kuhakikisha mazingira yanabaki salama kutokana na uharibifu uliokithiri. “Suala la matumizi ya nishati safi katika kata yetu linafanyika kwa weledi mkubwa sana, tunatumia mikutano ya hadhara kuelimisha wananchi kwasababu ndio mahali rahisi kukutana na wananchi kwa wakati mmoja. Nishati safi ina faida nyingi ikiwemo kuokoa muda, inatunza mazingira na kukuza uchumi. Tupo katika harakati za kupunguza matumizi ya mkaa kwa watu wetu wa hapa mjini na matumizi ya mkaa na kuni kwa wananchi waishio pembezoni mwa kata yetu” alisema Mwansasu.
Aliongeza kuwa kampeni ya nishati safi ilichagizwa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde kwa kugawa majiko ya gesi ikiwa ni motisha ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa wananchi.
Kwa upande mwingine Mkuu wa Shule ya Sekondari Kikuyu, Mwl. Gasper Mmary alieleza namna ambavyo matumizi ya nishati safi yanavyotumika katika shule yake pamoja na faida zake. “Shule yetu ya sekondari pia ipo bega kwa bega katika kumuunga mkono rais wetu hasa katika matumizi ya nishati safi. Kwanza kabisa matumizi ya nishati safi yanarahisisha kupika. Hapo awali tulikuwa tukitumia mkaa kupikia, baada ya ujio wa nishati safi katika shule yangu imeturahisishia kwa kiasi kikubwa kwa sababu hakuna uchafuzi wa hali ya hewa” alisema Mwl. Mmary.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.