MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde (wa pili kutoka kushoto pichani juu) ameonesha dhamira yake ya kuboresha sekta ya Elimu Jijini Dodoma kwa kuweka mpango mkakati wa kuziwezesha Computer na Printer Shule zote 134 za umma za Sekondari na msingi katika Jiji la Dodoma ili kurahisisha uratibu wa shughuli za ofisi na uchapaji mitihani.
Mavunde ameyasema hayo leo katika mahafali ya Kidato cha IV yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Chinangali,Dodoma ambapo jumla ya wanafunzi 239 walikuwa wanaagwa rasmi leo kabla ya kujiandaa na mitihani ya mwisho ya Taifa Novemba 2021.
“Dhamira yangu ni kuona tunafanya mapinduzi makubwa ya elimu kutumia teknolojia ya habari,ndio maana kipindi cha miaka minne iliyopita niligawa vishkwambi (Tablets) kwa shule za msingi 20 ambavyo vina thamani ya Tsh 1.7 bilioni ambavyo vimeleta mapinduzi makubwa sana kwenye ufundishaji.
Nataka kuwahakikishia kwamba nitagawa kompyuta na Printa kwa shule zote za Serikali 134 na tayari mpaka sasa nimeshazifikia shule 51 nitahakikisha nazimaliza zote ili watoto wetu wapate fursa ya kuweza kufanya mitihani yao ya wiki kwa urahisi.
Ninaamini kupitia maendeleo ya teknolojia na habari wanafunzi wengi wa Dodoma Jiji wataweza kufanya vizuri katika masomo yao ili kurudisha heshima ya Dodoma Jiji kitaaluma.” Alisema Mavunde.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Diwani wa Kata ya Chamwino Mh.Jumanne Ngede na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule Bw. Wenselaus Mkingule wameshukuru Mbunge Mavunde kwa ushirikiano mkubwa anaowapa katika uendelezaji wa Elimu katika shule hiyo na kumshukuru kwa nia yake thabiti ya kutengeneza uwanja wa mpira na kuweka magoli ya Chuma pamoja,kugawa jezi na kutunisha mfuko wa Shule kwa kuchangia Tsh 500,000.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.