Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo amesema kuwa atawatetea madaktari ambao watatimiza majukumu yao, lakini hatasita kuwachukulia hatua wale ambao wataenda kinyumbe na taratibu.
Waziri Jafo ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kilichofanyika jana katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma.
Mhe. Jafo amesema kuwa madaktari wamekuwa wakijitoa kwa weledi mkubwa katika kuwahudumia wananchi ili kuhakikisha kuwa wanatoa huduma bora kwa jamii na kuleta mabadiliko katika sekta ya afya nchini.
“kuna watu wanafanyakazi usiku na mchana tusipowalinda watu wanaofanyakazi tutawaumiza, siamini kama kweli mtumishi mmoja pekee anaweza kula fedha bila kuwa na ushirikiano na watu wengine, si kweli hata kidogo, tutende haki kwa watumishi wanaotoa huduma za afya nchini” Amesisitiza Mhe. Jafo
Amesema Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanaofanya vibaya wanapaswa kuadhibiwa lakini lazima haki itendeke katika kuwachukulia hatua ili kuleta usawa na kupunguza malalamiko kwa wataalam wa afya nchini.
Amewaagiza viongozi wa Halmashauri kutenda haki wakati wa kuwachukulia hatua watumishi kwa kufuata sheria na taratibu za utumishi wa umma na kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa kina wa tuhuma zilizotolewa dhidi yao ili kujiridhisha ndipo watoe maamuzi yaliyosahihi.
Mhe. Jafo amefafanua kuwa kumekuwepo na tabia ya baadhi ya viongozi kuwashusha madaraka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya bila kufuata sheria na taratibu za kiutumishi kwa kusikiliza majungu na uongo usiofanyiwa kazi jambo hili si haki, hivyo serikali itaendelea kuwatetea na kuhakikisha wanarudishwa kwenye nafasi zao.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema kuwa Serikali imejenga miundombinu ya huduma za afya ambapo mpaka sasa vituo 470 vimekarabatiwa na kujengwa nchini kwa gharama ya shilingi bilioni 321.
Mhandisi Nyamhanga amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanasimamia utoaji wa huduma bora za afya kwa watumishi ili waweze kufanyakazi kwa bidi na kuhakikisha huduma za afya zinaboreka nchini.
Wakati huohuo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo na Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndungulile amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanaweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha watumishi walio chini yao wanatoa huduma bora kwa jamii ili kuwavutia kupata huduma hiyo kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya vilivyojengwa nchini.
Pia, aliwataka kuweka mikakati ya kuimarisha hali ya lishe katika ngazi ya jamii ili kupunguza hali ya udumavu kwa wananchi.
Aidha Katibu Mkuu wa Afya, Maendeleo na Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainabu Chaula amewataka Waganga hao wa Mikoa na Wilaya nchini kuhakikisha wanafanyakazi kama timu kwa kudumisha umoja na ushirikiano ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa jamii zinakuwa bora nchini.
Chanzo: Tovuti ya tamisemi (www.tamisemi.go.tz)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.