NSSF kufanya uwekezaji wa zaidi ya bilioni 148 Dodoma
Imewekwa tarehe: December 26th, 2024
Na. Hellen M. Minja,
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), unatarajia kuanzisha uwekezaji ndani ya Makao makuu ya Nchi (Mkoa wa Dodoma) kwa kujenga jengo la ghorofa 16 ,jengo ambalo gharama yake inakadiriwa kuwa zaidi ya shilingi za Kitanzania Bilioni 148 likijumuisha hoteli yenye hadhi ya nyota tano.
Hayo yameelezwa wakati wa hafla ya upandaji miti kwenye eneo lao la uwekezaji lililopo Njedegwa Jijini Dodoma ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alikua mgeni rasmi.
“Hoteli hii itafungua fursa mpya ya kufanyika mikutano ya Kimataifa hapa Dodoma hivyo kuongeza mnyororo wa thamani pia itachangia kukuza utalii na kuzalisha ajira zaidi pamoja na kupendezesha Jiji letu la Dodoma. Niwapongeze kwa kuunga mkono juhudi za utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti leo hata kabla hamujaanza mradi”. Amesema Mhe. Senyamule.
Kadhalika, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Bw. Masha Mshomba, amesema suala la uwekezaji ni jukumu la kipekee na linatakiwa kufanyika kwa umakini mkubwa ili kuleta kipato cha kutosha kwa kuwa fedha hizo ni za wananchi.
Akielezea namna mradi utakavyotekelezwa, Meneja Usimamizi wa Mradi NSSF, Mhandisi Helmes Pantaleo amesema;
“Mradi unatarajiwa kuwa na jengo la ghorofa 16 na umegawanyika katika sehemu tatu, kuna eneo la ofisi, hoteli na mall, eneo hilo lina ukubwa wa zaidi ya mita za mraba 20,000, na eneo zima la uwekezaji lina ukubwa wa hekta 2.1, hoteli itakua na vyumba 20 pamoja na migahawa, maduka na ofisi za watu wa hoteli”
Mradi huo unaotarajiwa kutumia miaka mitatu (2025 - 2028 ) hadi kukamilika kwake,utaanza kutekelezwa mwezi Mei 2025, vibali vya ujenzi vimeshapatikana kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Ofisi ya Waziri Mkuu, Msajili wa majengo na Wizara ya Fedha, hivvyo kufikia Aprili 2O25 maandalizi yote yatakuwa yamekamika.