HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imewaondolea hofu wananchi wa Kata ya Nzuguni ya kubomolewa makazi yao kutokana na ujenzi usiozingatia taratibu za Mipango Miji baada ya kukamilisha zoezi la upimaji shirikishi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la hilo Godwin Kunambi alipokuwa akiongea na wananchi wa Kata hiyo iliyopo Jijini hapa jana baada ya kukamilika kwa zoezi la upimaji shirikishi eneo la Nzuguni ‘A’.
Kunambi alisema “kwanza napenda kuwapongeza wataalam wangu kwa kazi nzuri mliyoifanya ya upimaji shirikishi katika eneo za Nzuguni A, kupitia zoezi hilo la upimaji shirikishi, hofu kwa wananchi imeondolewa, kwamba kesho watabomolewa makazi yao”.
Kunambi alisema zoezi hilo limetekelezwa na Halmashauri kwa lengo la kuwahakikishia wananchi makazi bora na salama kwa mujibu wa taratibu za Mipango Miji.
Akiongelea umuhimu wa zoezi hilo, Kunambi alisema kuwa kukamilika kwa zoezi la upimaji shirikishi kutawawezesha wananchi kupata hati halali za umiliki wa viwanja ambazo zitawawezesha kupata mikopo katika taasisi mbalimbali za kifedha na kwamba Halmashauri ya Jiji inadhamira ya kuona wananchi wake wanaishi katika makazi bora na kuwa na uwezo wa kifedha kupitia rasilimali zao ikiwemo ardhi.
Akiongelea migogoro ya mipaka kwa baadhi ya wananchi, Mkurugenzi huyo aliwahakikishia wananchi hao kuwa timu ya wataalam wa kutosha kutoka Halmashauri wataweka kambi katika Kata ya Nzuguni ili kuhakikisha wananchi wote wenye changamoto wanahudumiwa na kugawiwa viwanja kwa mujibu wa taratibu.
Naye msimamizi wa mradi wa upimaji shirikishi Nzuguni A, Aisha Masanja alisema kuwa mradi huo utahudumia wananchi 5,942 ukiwa na jumla ya viwanja 11,160 vya matumizi mbalimbali.
Akiongelea faida za mradi huo, Masanja alisema kuwa mradi huo utawawezesha wananchi kujenga katika viwanja vilivyopimwa na kuwawezesha kupata hati za umiliki wa viwanja hivyo.
“Halmashauri ya Jiji itafungua barabara zote katika eneo la mradi wa Nzuguni A na kujenga huduma za kijamii kama shule, vituo vya afya na viwanja vya michezo” alisema Masanja.
Alizitaja faida nyingine kuwa ni kupanga Mji kwani Halmashauri itakabiliwa na tatizo la makazi holela iwapo mji utaachwa bila kupangwa na kusisitiza upimaji huo unaondoa tatizo la makazi holela na vilevile, upimaji huo utatatua tatizo la migogoro ya mipaka inayolalamikiwa na wananchi.
Baadhi ya wakazi wa Nzuguni A akiwemo Wilfred Chimosa wamepongeza juhudi za Serikali za kufanya upimaji shirikishi katika eneo hilo.
“Shukrani kwa taarifa iliyowasilishwa na Afisa wa Halmashauri kwani inaonesha kazi nzuri iliyofanywa na Halmashauri ya Jiji…Moyo wangu sasa umesuuzika na nawashukuru sana Halmashauri ya Jiji kwa kazi nzuri” alisema Chimosa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, David Bochela aliwataka wananchi wa Kata ya Nzuguni kusimamia maamuzi halali yaliyoamuliwa kuhusiana na mradi huo.
“Simamieni mlichoamua, nashauri mapungufu ya watu wachache wenye migogoro ya ardhi yatatuliwe kwa utaratibu uliowekwa, na waale ambao haturidhiki tusicheleweshe wengine kwa maslahi yetu” alisema Bochela ambaye ni Diwani wa Kata ya Mkonze Jijini humo.
Aidha, aliwataka wananchi hao kujikita kwenye shughuli za maendeleo kuliko kuzalisha migogoro isiyo na tija.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.