Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
Timu ya Ofisi ya Rais Ikulu kuvuta Kamba (wanaume) imeibuka na ushindi wa alama 2-0 dhidi ya Timu ya Ofisi ya Rais Jiji Dodoma kuvuta Kamba (wanaume) katika upande wa wanawake Timu ya Ofisi ya Rais Ikulu ikiibuka na ushindi wa alama 2-0 dhidi Timu ya Ofisi ya Rais Jiji Dodoma katika mchezo huo.
Mchezo huo ulifanyika ndani ya Uwanja wa Jamhuri katika Bonanza la Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma lililohusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, michezo ya jadi na tamasha la sanaa.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Michezo, Utamaduni na Sanaa Jiji la Dodoma, Patrick Moshi, aliwataka washiriki wa michezo mbalimbali kujiamini zaidi wawapo uwanjani ikiwa ni njia kufanikiwa na kupata ushindi katika michezo yao. “Siri ni kufanya mazoezi mapema na wakati wa mchezo ni kujiamini zaidi na hiyo ndio siri ya mafanikio” alisemaMoshi.
Mwamuzi wa mchezo wa kuvuta kamba, Idrisa Shabani aliwaomba washiriki wa michezo mbalimbali kuwa na tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuwajengea uwezo wa kukabiriana ipasavyo pindi wanapokuwa kwenye michuano na timu pinzani. “Watu waje kufanya mazoezi, kama tunavyoona Timu ya Ofisi ya Rais Ikulu ilikuwa imejipanga kwa kufanya mazoezi lakini Timu ya Ofisi ya Rais Jiji Dodoma ilikuwa haijajipanga na ndio maana wamefungwa” alisema Shabani.
Akizungumzia kuhusu mchezo huo wa kuvuta kamba, mmoja kati ya washiriki kutoka Timu ya Ofisi ya Rais Jiji Dodoma, Devotha Selufara, alisema amefurahishwa na kuwepo kwa michuano hiyo na kuomba michezo hiyo iwe endelevu ili kuendelea kuimarisha afya kimwili na kiakili. “Ninaomba zoezi hili lisiishie hapa, lijirudie ili tuwe tunafanya mazoezi mara kwa mara kwasababu ina imarisha viungo vyetu lakini pia afya zetu zinakuwa salama” alisema Selufara.
Nae, shabiki na mpenzi wa mchezo wa kuvuta kamba, Perpetua Mtega, aliwaasa washiriki wa michezo mbalimbali kutokuwa na tabia ya kukata tamaa hasa pale wanapopoteza katika michuano hiyo kwasababu katika mchezo wowote lazima apatikane mshindi na asiyekubari kushindwa siyo mshindani. “Nimefurahi kwa sababu wachezaji wote wamejiamini, wamejitoa na walikuwa tayari kupokea ushindi hivyo sina budi kusema kwamba popote kunapokuwa na ushindani lazima apatikane mshindi mmoja” alisema Mtega.
Ushindi wa wachezaji katika michezo mbalimbali hutegemea sana maandalizi mazuri ya awali, uthubutu, kujiamini na bidii ya kutosha ili kuepuka kuteteleka ndani ya mchezo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.