Na. Dennis Gondwe, DODOMA
VITUO vya Afya katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma vimetakiwa kupanda miti ili kutunza mazingira na kuwahakikishia wananchi mazingira bora ya huduma.
Agizo hilo lilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipoongoza Timu ya Menejimenti ya halmashauri yake kutembelea na kukagua hatua ya ujenzi wa vituo vya afya vinavyojengwa katika halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa lilifanyika zoezi la kupanda miti katika maeneo ya kituo cha Afya Chang’ombe lakini iliachwa ikaharibika. “Miti yote iliyopandwa na kuharibika ipandwe tena ili kufikia lengo la awali la upandwaji wake. Wananchi wanahitaji huduma bora za afya katika mazingira safi na yenye kivuli. Tukiacha eneo hili bila miti kituo cha afya kitageuka jangwa” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Awali Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alisema kuwa ilipandwa miti 54 kwa lengo la kutunza na kuhifadhi mandhari ya kituo hicho. Miti ya aina mbalimbali ilipandwa kwa lengo la kukifanya kituo kiwe na mandhari nzuri na ya kuvutia kwa wagonjwa.
Aidha, alisema kuwa kituo hicho kilipokea shilingi milioni 250,000,000 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa majengo mawili na kichomea taka. Aliyataja majengo hayo kuwa ni jengo la wagonjwa wa nje na jengo la maabara.
Kituo cha Afya Chang’ombe kimejengwa katika Kata ya Chang’ombe katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kikitarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya 25,000.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.