WAKAZI wa Jiji la Dodoma wameshauriwa kutumia bidhaa za kusindikwa za kampuni ya Pax kwa kuwa zinatengenezwa katika viwango vinavyozingatia ubora na usafi kwa afya ya mlaji.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa kampuni ya Pax inayotengeneza bidhaa za kusindika, Upendo Koshuma katika banda la SIDO kwenye maonesho ya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma.
Koshuma alisema kuwa bidhaa zinazosindikwa na kampuni yake zinatengenezwa kwa kuzingatia ubora na usafi wa hali ya juu kwa lengo la kuhakikisha afya ya mlaji inalindwa katika Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi. “Kampuni ya bidhaa za kusindikwa ya Pax inatengeneza bidhaa za aina tatu, karanga zilizosagwa ‘peanut butter’ asali na pilipili. Nikiongelea bidhaa ya karanga tunayosindika, ni tofauti ya bidhaa nyingine kwa sababu haiwekewi kitu chochote zaidi ya chumvi. Katika kuandaa bidhaa hii, tunazingatia mazingira ya usafi na kuhakikisha hakuna hata mchanga unaoingia ili kutokumsababishia usumbufu mlaji” alisema Koshuma.
Kuhusu asali, alisema kuwa kampuni yake hununua asali kutoka kwa wakulima baada ya kujiridhisha kuwa asali hiyo imefikia viwango vya ubora vinavyokubalika na ni salama kwa mlaji. “Tukishajiridhisha kuwa asali hiyo ni salama kutoka kwa wakulima, tunaichuja, kuiandaa na kuipaki vizuri kabla haijakufikia mteja wetu ili upate bidhaa yenye ubora. Kwa upande wa pilipili, tunatengeneza pilipili ambayo inachanganywa na karoti, kitunguu swaumu na kitunguu maji” alisema Koshuma.
Aidha, aliwaalika wananchi wanaofika katika maonesho ya Nanenane kutembelea bidhaa zake zinapopatikana chini ya mwamvuli wa SIDO.
Maonesho ya Nanenane mwaka 2020 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, chagua viongozi bora 2020”.
Upendo Koshuma wa kampuni ya Pax akionesha bidhaa za Karanga na Asali zinazosindikwa na kampuni yao.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.