Na. Sifa Stanley, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kununua mitambo miwili ambayo ni "Buldoza na Greda" kwa ajili ya kufungua na kuchonga barabara katika maeneo ambayo yalikuwa sio rahisi kufikika.
Pongezi hizo alizitoa wakati wa zoezi la ufunguzi na uzinduzi mdogo wa mitambo iliyonunuliwa na Jiji la Dodoma leo katika eneo la Low Coast Kata ya Kizota.
Mkuu huyo alisema kuwa mitambo hiyo itakwenda kuongeza thamani ya maeneo na kusaidia maeneo yaliyokuwa hayafikiki kwa urahisi hapo awali kuweza kufikika.
“Mitambo hii inakwenda kuongeza thamani ya maeneo watu walio wengi huingia uzito wa kuendeleza maeneo yao kwasababu hayafikiki, wakipeleka nondo, wakipeleka mchanga malori yanakuwa yanazama kwahiyo barabara zinakwenda kurahisisha mambo hayo na kuongeza thamani ya maeneo” alisema Shekimweri.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alieleza namna jiji la Dodoma litakavyonufaika kutokana na ununuzi wa mitambo hiyo, ambayo itatumika kufungua barabara zilizokuwa hazipitiki lakini pia jiji litakodisha mitambo hiyo na kujiingizia mapato.
“Mitambo hii ni chanzo kikubwa cha mapato, sisi kama jiji la Dodoma tumekuwa tukihangaika kupata vyanzo vipya vya mapato, nahii ni sehemu ya chanzo cha mapato, tukishahakikisha tumewachongea wananchi barabara, mitambo hii haitabaki hapa bure, tutaikodisha kwa wakandandarasi wanaofanya ujenzi wa barabara na itaingiza milioni 40 kwa mwaka” alisema Mafuru.
Aidha, Naibu Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Jamal Ngalya alieleza namna Halmashauri ya Jiji ilivyojipanga kuhakikisha kuwa mitambo hiyo inatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na aliahidi mitambo hiyo kutunzwa vizuri.
“...kwa niaba ya madiwani wa Halmashuri ya Jiji la Dodoma, tuahidi usimamizi mzuri wa mitambo, tukuahidi mitambo tutaisimamia vizuri na kila siku tutabuni nini cha kufanya juu ya mitambo yetu” alisema Ngalya.
Mkuu wa Wilaya amezindua mitambo yenye gharama ya shilingi bilioni 1.5 ambapo fedha hizo ni mapato ya ndani ya jiji la Dodoma, mitambo hiyo itatumika kuchonga na kufungua barabara katika maeneo ambayo yalikuwa hayafikiki kwa urahisi hapo awali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.