Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri (wa katikati pichani juu) amempongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru kwa kutoa shilingi 12,000,000 kutatua changamoto ya usafirishaji wa vifaa wakati wa mvua kuvipeleka kwenye mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari Hombolo Makulu.
Pongezi hizo alizitoa wakati akimkaribisha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Dodoma kutembelea na kukagua shule hiyo.
Shekimweri alisema kuwa “na mimi nichukue nafasi hii kwa dhati kabisa nimpongeze hadharani Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru. Mmepokea hapa taarifa, mmepokea changamoto lakini hazikusemwa vizuri huyu, mkurugenzi ameingia mfukoni kwake ametoa shilingi 12,000,000 kusaidia changamoto ya usafirishaji vifaa wakati ule wa mvua. Mafuru mimi nakupongeza sana. Sisi tunatamani Jiji la Dodoma liwe la mfano kwenye kutekeleza miradi, tunataka kuwa ‘center of excellency’ kwenye utekelezaji wa miradi alisema Shekimweri.
Mkuu huyo wa wilaya aliipongeza kamati ya ujenzi na walimu kwa kusimamia vizuri ujenzi wa shule hiyo. Alisema kuwa ushirikiano huo ndiyo umefanikisha kupiga hatua kubwa katika ujenzi huo.
Mradi huu utaajiri watu wengi. “Ajira ya mara moja inayoonekana ni ya walimu. Lakini tuna maabara, lazima tutaajiri wataalam wa maabara, tutakuwa na mafundi wateknolojia wa maabara. Lazima tuajiri mkutubi na wasaidizi, mpishi, boharia na mhasibu wa shule na ulinzi. Hivyo, ajira unaizungumzia katika mapana hayo. Kuna watakaoajiriwa ndani ya Hombolo Makulu na nje ya eneo hili” alisema Shekimweri.
Ujenzi wa shule ya sekondari katika kata ya hombolo makulu ulianza tarehe 25 Januari, 2022 kwa fedha kutoka mradi wa kuboresha elimu ya sekondari (SEQUIP) kwa gharama ya shilingi 600,000,000.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.