MAFANIKIO ya maendeleo yaliyopatikana katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma yametokana na utulivu wa madiwani na wataalam katika kupanga, kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe wakati wa majumuisho ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutembelea na kukagua miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma mwishoni mwa wiki.
Prof. Mwamfupe alisema kuwa mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo yanatokana na utulivu na kuelewana baina ya Baraza la Madiwani na wataalam wa Halmashauri. “Tumeona ishara ya mafanikio hapa. Mafanikio haya ambayo tumeyapata hakika yanatokana na Halmashauri ambayo ndani yake watu wametulia. Waheshimiwa Madiwani na wataalam wakiwa na utulivu, maendeleo tunakuwa na uhakika nayo. Tusipokuwa na utulivu hakuna maendeleo. Waheshimiwa madiwani wameshiriki kwa namna kubwa kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa hii miradi” alisema, Prof. Mwamfupe.
Akiongelea utekelezaji wa ujenzi wa miradi hiyo ya kimkakati, Meya huyo aliwapongeza wakandarasi kwa kazi nzuri. “Niwashukuru sana wakandarasi hawa, wamefanya kazi kubwa na nzuri. Wamefanya vitu vingine hata vya nyongeza nje ya kile tulichokubaliana kwa lengo la kuhakikisha dhamira njema inafikiwa” alisema Prof. Mwamfupe.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.