BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma leo tarehe 10 Disemba, 2020 limefanya Mkutano wa kwanza katika ukumbi mkuu wa Halmashauri hiyo na kumchagua Diwani wa Kata ya Madukani kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Prof. Davis Mwamfupe (pichani juu) kwa jumla ya kura 54 kati ya 54 zilizopigwa, hivyo kumfanya kushinda tena kiti cha Meya wa Halmashauri ya Jiji hilo kwa muhula mwingine wa miaka mitano.
Aidha Baraza hilo limemchagua Diwani wa Kata ya Matumbulu Mhe. Emmanuel Chibago kuwa Naibu Meya, kwa kura 54 kati ya 54 zilizopigwa.
Akiongea baada ya ushindi huo, Mhe. Prof. Mwamfupe alitoa shukrani za dhati kwa Chama chake na Madiwani wote waliomuamini na kumpigia kura na kuahidi kushirikiana nao katika kuwatumikia wananchi wa Jiji la Dodoma kwa lengo la kuwaletea maendeleo.
"Niwashukuru sana waheshimiwa Madiwani kwa kunichagua, ninachokiomba kwenu ni ushirikiano, tukishirikiana hakuna jambo litakalotupa shida, nawashukuru viongozi kwa kusimamia kanuni, na ninaahidi kuongoza kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa bila ubaguzi wala upendeleo wa aina yoyote." Alisema Prof. Mwamfupe.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Josephat Maganga alisema kuwa uchaguzi umeisha na kazi inayofuata ni ya Madiwani kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria kanuni na maelekezo.
Maganga amewaomba waheshimiwa Madiwani hao kujadili mambo yatakayoleta tija katika Kata zao na Jiji kwa ujumla kama vile masuala ya miundombinu ya barabara, afya na elimu, na yeye kama Mkuu wa Wilaya atakuwa mstari wa mbele kuwapa ushirikiano katika utekelezaji wa masuala yatakayoleta maendeleo Jijini hapa.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Joseph Mafuru alimpongeza Meya na Naibu wake kwa ushindi wa kishindo pamoja na waheshimiwa Madiwani na kuwahakikishia kuwa yale yote watakayokua wanajadiliana kwenye vikao watayatekeleza kwa wakati na kwa ufanisi wa hali ya juu.
"Mimi na timu yangu niwaahidi kitu kimoja kuwa tupo tayari kushirikiana nanyi waheshimiwa Madiwani ili kuleta maendeleo katika Jiji letu la Dodoma kwani kazi yetu kubwa ya kwanza ni kutoa huduma kwa wanachi wetu kama Halmashauri nyingine, lakini pili tunakazi ya kustawisha Makao Makuu ya nchi hivyo tukishirikiana tutawaletea maendeleo wananchi wetu na Taifa kwa ujumla." Alisema Mafuru.
Mhe. Prof. Devis Mwamfupe na Mhe. Emmanuel Chibago (kushoto) kabla ya uchaguzi ambapo wote wamechaguliwa na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuendelea na vyadhifa walizokuwa wakizishikilia kabla ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Mhe. Josephat Maganga akitoa nasaha zake mbele ya Madiwani (hawapo pichani).
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru akiongea kutoa ahadi ya timu yake ya menejimenti kutoa ushirikiano kwa madiwani ili kuhakikisha Jiji linazidi kupiga hatua katika maendeleo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.