SHIRIKA la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN Women) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) wanatekeleza mradi wenye lengo la kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 49 katika maeneo ya wazi na mikusanyiko kama Masoko, Baa, Shule, na Taasisi mbalimbali za Umma ambapo suala la wanawake kushikwa bila ridhaa yao linaelezwa kama kikwazo na changamoto kubwa.
Akifungua warsha ya siku moja ya kuhamasisha jamii kuhusu jitihada za kuzuia na kupambana na unyanyasaji huo katika ukumbi wa Jiji jana, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe alisema Wanawake na Watoto wanafanyiwa matukio mengi ya kikatili kama vile kushikwashikwa miili yao na kuzomewa kwa sababu ya maumbile yao.
Alisema kwa sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo visivyofaa katika jamii ikiwemo ulevi uliopindukia, utumiaji wa dawa za kulevya hasa bangi, ukabaji na uporaji pamoja na uvaaji wa mavazi yasiyozingatia maadili na kwamba vyote hivyo vinachangia katika ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
“Tutambue kuwa wanawake na watoto wanakutana na matukio mengi ya ukatili, unyanyasaji, na kufanyiwa vitendo visivyofaa…hili linathibitishwa na tafiti mbalimbali ikiwemo ule wa ‘Tanzania Demographic Survey’ wa mwaka 2015/2016 unaoonyesha kuwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 49 umefikia Asilimia 40” alisema Mwamfupe katika hotuba yake.
Aidha, Mwamfupe alisema kuwa wanawake wengine wanadhalilishwa kutokana na maumbile yao, jambo ambalo ni kikwazo kwa uhuru dhidi yao, na kwamba ni wakati kwa jamii nzima kupaza sauti ya kupambana na hali hii kwani athari zake ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya Wanawake na Watoto ikiwemo kupata fursa za Elimu na kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Akizungumza wakati wa warsha hiyo, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Mwajina Lipinga alisema kuna haja ya kuweka Sheria ndogo zitakazoshughulikia matukio kama haya.
“Tuna haja ya kufikiria tuweke Sheria ndogo ambazo zitasaidia kudhibiti kwenye haya maeneo kuzuia vitendo vya ukatili visitokee na kudhibiti pale yanapotokea” alisema Mwajina.
Mradi huo ambao unatarajiwa kupambana na hali hiyo, unatekelezwa katika Mikoa ya Dodoma na Shinyanga kama maeneo ya kuanzia, ambapo warsha ya uhamasishaji ilijumuisha baadhi ya Madiwani, baadhi ya Maofisa Watendaji wa Kata, Baadhi ya Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Baadhi ya Maofisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya Kata, Wawakilishi wa Wanawake wanaofanya biashara katika Masoko, Viongozi wa Masoko, na Wawakilishi wa vikundi vya Wanaume wanaofanya biashara katika Masoko.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.