HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imepata Meya mpya kufuatia uchaguzi uliofanyika leo Julai 19, 2017 katika Ukumbi wa Manispaa hiyo ambapo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Profesa Davis George Mwamfupe ameshinda nafasi hiyo.
Profesa Mwamfupe ameshinda nafasi hiyo kwa kupata kura 50 kati ya kura zote 58 zilizopigwa na wajumbe 58, dhidi ya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kikombo katika Manispaa hiyo Yona Kusaja aliyepata kura 8.
Awali, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ambaye pia ndiye Msimamizi wa Uchaguzi aliwaeleza wajumbe utaratibu mzima wa kupiga kura kwa njia ya siri kwa kutumia karatasi maalum za kupigia kura, na kwamba wajumbe halali watakaopiga kura kwa mujibu wa sheria ni Madiwani wa Manispaa ya Dodoma tu.
Baada zoezi la kupiga na kuhesabu kura kukamilika, Msimamizi wa Uchaguzi Godwin Kunambi kwa Mamlaka aliyonayo kisheria, alimtangaza rasmi Profesa Mwafupe kuwa mshindi na kwamba ndiye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma.
Uchaguzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Anthony Mavunde, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Felister Bura, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma Balozi Job Lusinde, wataalam wa Manispaa ya Dodoma na Wakazi wa Manispaa wa Dodoma.
Profesa Mwamfupe anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Meya mheshimiwa Jaffar Mwanyemba ambaye aliondolewa madarakani na Baraza la Madiwani Aprili 3 mwaka huu kwa kupigiwa kura za kutokuwa na imani naye kufuatia tuhuma za matumizi mabaya ya Ofisi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.