RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amewapa wiki moja mabalozi aliowateua na kuwaapisha leo, wawe wamewasili vituo vyao vya kazi katika nchi wanazowakilisha na kuchapa kazi.
Kauli hiyo ameitoa muda mfupi baada ya kuwaapisha katika Ikulu ya Chamwino iliyopo Dodoma leo asubuhi.
Rais Dkt. Magufuli ametoa wiki moja kwa mabalozi hao kuwa wameondoka Tanzania kwenda kufanya kazi katika nchi walizopangiwa. Kauli hiyo inafuatia tabia iliyokuwa ikifanywa na baadhi ya mabalozi wanapoapishwa badala ya kwenda katika nchi walizopangiwa wanatumia muda mrefu nchini kabla ya kuondoka.
Wakati huohuo, Rais amewapongeza mabalozi hao ambao ni mabalozi wa kwanza kuapishwa Ikulu ya Chamwino Dodoma na kutaka utendaji kazi wao ukaakisi Makao Makuu ya nchi. “Nendeni mkamtangulize Mungu katika kazi zenu, nawatakia mafanikio mema” alimalizia Rais.
Katika hatua nyingine, Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka mabalozi walioapishwa leo kutambua kuwa Tanzania ina maslahi katika nchi wanazokwenda kuwakilisha. Aliwakumbusha kuwa dhamira ya nchi ni kufikia uchumi wa viwanda. “kupitia nyie tunaamini nchi hizo zitakwenda kuchangia katika uchumi wa viwanda. Nchi mnazokwenda kuna watanzania walio huko. Mkawatambue ili nao wahamasishwe kuisemea nchi yetu, kuilinda na kuitetea nchi yetu. Tunahitaji mchango wao ili kuimarisha maslahi ya nchi yetu” alisema Waziri mkuu Majaliwa.
Kwa upande wake, Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki Prof. Palamagamba Kabudi amewataka mabalozi walioapishwa leo kutunza uaminifu na imani ambayo Rais Dkt. John Magufuli amewapa. “Msivunje viapo vyenu na msiwe legelege” alisema Prof. Kabudi.
Naye Rais Magufuli, katika maneno machache aliyoyatoa baada ya hotuba ya Waziri Kabudi, alisema: “Najua mengi yameshasemwa, kwa kifupi napenda kuwapongeza mabalozi niliowaapisha leo, mkaiwakilishe nchi yetu vizuri na nawapongeza kwa kuwa ndiyo mabalozi wa kwanza kuapishwa hapa Ikulu ya Dodoma” amesisitiza Rais Magufuli.
Mabalozi walioapishwa na nchi zao kwenye mabano ni Balozi Maj. Gen Anselm Shigongo Bahati (Misri), Balozi Mohamed Abdallah Mtonga (Abu Dhabi), Balozi Jestas Abouk Nyamanga (Ubelgiji), Balozi Ali Jabir Mwadini (Saud Arabia) na Balozi Dkt. Jilly Elibariki Malebo (Burundi).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.