Rais wa Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza waislam wote nchini kwa kumaliza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na anawashukuru kwa namna walivyoshiriki kuliombea Taifa hasa katika kipindi hiki cha kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19.
Hayo yamesemwa leo (Jumapili, Mei 24, 2020) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akizungumza na waumini wa dini ya kiislam mara baada ya kumaliza kuswali salam ya Eid El Fitri katika msikiti wa Gaddafi, jijini Dodoma.
Pia Dkt. Magufuli amewashukuru waumini wa dini nyingine nchini kwa kushiriki kikamilifu kwenye kuliombea Taifa. "leo hii tunamaliza dua ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, jambo hili Mheshimiwa Rais anasema hatasahau kwa viongozi wote wa dini kuwa pamoja kuliombea Taifa. Pia Mheshimiwa Rais amesema tuendelee na dua zetu, kila mmoja kwa imani yake wakati wote ili Mwenyezi Mungu aendelee kutuondoa katika janga hili ambalo limeleta mtikisiko duniani kote."
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania wote kwa ujumla waendelee kushirikiana katika kulifanya Taifa liwe la amani na utulivu. "Dini zetu zinatutaka kila mmoja aendelee kuomba, nchi hii imekuwa na utulivu sana na mfano duniani kwa nchi zinazotaka amani."
"Tuendelee na tabia hii na viongozi wa dini endeleeni kusisitiza suala la amani, Serikali inawasisitiza muendelee na shughuli zenu, sisi tutahakikisha tunaendelea kulinda amani, fanyeni kazi, mkulima lima na kwa walio viwandani nao waendelee kufanya kazi." Kadhalika, Waziri Mkuu amesema wananchi wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa COVID-19, ambao amewasisitiza wasiwe na hofu na waendelee kufanya kazi kwa bidii.
Akizungumzia kuhusu hali ya ugonjwa wa COVID-19 ilivyo kwa sasa nchini, Waziri Mkuu amesema katika hospitali ya Amana yupo mgonjwa mmoja, Mloganzila yupo mmoja, Temeke hatuna mgonjwa aliyethibitishwa, Kairuki hakuna mgonjwa, Rabiansia hakuna mgonjwa, Regency hakuna mgonjwa, Aga Khan yuko mgonjwa mmoja, Lulanzi Kibaha wapo wagonjwa 16 na Dodoma Mkonze mpaka leo asubuhi wapo wagonjwa watatu.
Chanzo: maelezonews (instagram)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.