RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aahidi kuendelea kukuza uchumi na kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana, muda mfupi baada ya kula kiapo (pichani) kwa nafasi ya urais tukio lililofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma leo.
Rais, Dkt Mafuguli amesema kuwa jukumu alilonalo ni kukuza uchumi wa Watanzania na kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana. “Serikali ninayoiongoza itazidisha mapambana dhidi ya rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma” alisema Dkt. Magufuli.
Aidha, ameahidi kujenga uwanja mkubwa wa kisasa wa michezo jijini Dodoma. “Shukrani sana wana Dodoma kwa kuhudhuria kwa wingi kwenye tukio hili. Watu wameanza kuingia uwanjani usiku, nawashukuru kwa heshima hii kubwa mliyonipa na imedhihirisha kuwa Dodoma ndiyo Makao Makuu ya nchi. Serikali itakayoanza leo, kitu cha kwanza ni kujenga uwanja mkubwa wa michezo hapa Dodoma ili sherehe zijazo watu wote wa Dodoma wawe ndani ya uwanja washerehekee vizuri” alisema Rais, Dkt. Magufuli.
Amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi kimepata ushindi mkubwa kutokana na baraka za wana Dodoma kwa sababu uzinduzi na kilele cha kampeni za uchaguzi mkuu zilifanyika Jijini Dodoma. “Yote tuliyoahidi tutayashughulikia ikiwemo ujenzi wa barabara ya mzunguko, sababu msongamano umeanza kuonekana Dodoma” aliongeza Rais huyo.
Akitoa salamu kwa niaba ya wananchi wa Jamhuri ya Comoro, Rais wa nchi hiyo, Azali Assoumani alimuomba Mungu kumsaidia sana Rais, Dkt. Magufuli kutekeleza kazi aliyopewa na watanzania kwa ufanisi.
“Nachukua nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Tanzania kukamilisha salama mchakato wa uchaguzi, nawashukuru kwa uwepo wao hapa. Tunashukuru kila tunapokuja Tanzania mimi na ujumbe wangu tunapokelewa vizuri na kujisikia tupo nyumbani” alisema Rais Assoumani.
Nae, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa alisema “naleta salamu nyingi kutoka kwa wananchi wa Zimbabwe. Tunamshukuru Rais, Dkt. Magufuli alifanya ziara nchini Zimbabwe. Na wakati wa ukame mkali, Rais Dkt. Magufuli alitupatia msaada wa mahindi kwa Wazimbabwe. Huyu ni kiongozi mzalendo katika ukanda huu”.
Wakati huohuo, Mwanazuoni na Mhadhiri wa Sheria kutoka Kenya, Prof. Patrick Loch Otieno Lumumba kupitia televisheni ya TBC amempongeza Rais, Dkt. Magufuli na CCM kwa ushindi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Prof. Lumumba ametoa tahadhari kuwa makini na wafadhili wavurugaji nchi za kiafrika. “Katika nchi za kiafrika, tuwe wepesi kujiepusha na wafadhili wenye lengo la kuvuruga nchi za Afrika. Tatizo la nchi za Afrika ni kutotofautisha upinzani na ubabaishaji. Tuhakikishe tunaendesha siasa ambazo zinalinda usalama wetu” amesema Prof. Lumumba kwa msisitizo.
Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ameapishwa leo katika sherehe za aina yake zilizofanyika kwa mara ya kwanza Jijini Dodoma katika uwanja wa Jamhuri tangu Dodoma kupata hadhi ya Jiji na kuwa Makao Makuu ya nchi.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akila kiapo kushika nafasi hiyo kwa miaka mingine mitano.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.