RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 16 Novemba, 2020 amemuapisha Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli pia amewaapisha Mawaziri 2 aliowateua hivi karibuni katika Baraza lake jipya la Mawaziri ambao ni Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi aliyeapishwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Dkt. Philip Isdor Mpango aliyeapishwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Halfa ya uapisho huo imefanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Hussein Ali Mwinyi, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson.
Wengine ni Mawaziri Wakuu Wastaafu, Maspika Wastaafu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Adelardus Kilangi, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wa Dini, viongozi wa Vyama vya siasa pamoja na viongozi na watumishi wa Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Rais Magufuli amewataka Wabunge kutulia wakati akiendelea na mchakato wa uteuzi wa Mawaziri watakaounda Baraza la Mawaziri kwa kuwa ameamua kupitia kwa umakini mkubwa orodha ya Wabunge wote takribani 350 ili kupata wachache atakaowateua kuwa Mawaziri.
Mhe. Rais Magufuli ameeleza dhamira yake ya kutaka Serikali ifanye kazi zaidi katika kipindi chake cha pili cha uongozi kwa kuwa anatambua kuwa Watanzania wana imani na matumaini makubwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho wamekichagua kwa ushindi mkubwa na wa kihistoria kwa Tanzania Bara na Zanzibar, hivyo anataka viongozi ambao atawateua wawe na uwezo wa kweli wa kutimiza matarajio hayo ya wananchi.
Kuwa upande wake, Mhe. Waziri Mkuu Majaliwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa imani kubwa aliyoiondesha kwake na ameahidi kutekeleza wajibu wake kwa nguvu zaidi pamoja na kumshauri ipasavyo, na kwa kuanzia ameahidi kuchukua hatua mara moja dhidi ya upandishaji wa bei ya Saruji uliojitokeza siku chacha zilizopita.
Halil kadharika, Mhe. Waziri Kabudi na Mhe. Waziri Mpango wameahidi kutekeleza wajibu wao kwa nguvu zaidi na kwa kugusa zaidi mahitaji ya wananchi, hasa baada ya kupata uzoefu wakati wakigombea katika majimbo ambako wamechaguliwa kuwa Wabunge katika uchaguzi mkuu uliopita.
Chanzo:Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU Gerson Msigwa - Chamwino
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.