Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 07 Desemba, 2019 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi lenye urefu wa kilometa 3.2 na upana wa mita 28.45 litakalounganisha mawasiliano ya barabara kati ya Mikoa ya Mwanza na Geita kukatisha Ziwa Victoria.
Sherehe za uwekaji jiwe la msingi zimefanyika katika eneo la Kigongo, Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza na kuhudhuriwa na wananchi na viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera, Wabunge, viongozi wa taasisi mbalimbali, viongozi wa Dini na viongozi wa vyama vya siasa.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.66 umepangwa kukamilika mwezi Julai 2023 kwa gharama ya jumla ya shilingi Bilioni 699, fedha zote zinatolewa na Serikali ya Tanzania.
Daraja hilo refu kuliko yote Afrika Mashariki, na la 6 kwa urefu Barani Afrika litakuwa mbadala wa vivuko vya MV Misungwi, MV Sengerema na MV Mwanza, na litajengwa kwa teknolojia ya madaraja marefu inayoitwa Extra Dosed Bridge ambapo litajengwa juu ya nguzo 67 zikiwemo nguzo 3 zenye urefu wa meta 40 na umbali wa meta 160 kutoka nguzo moja hadi nyingine.
Mhandisi Mfugale amebainisha kuwa daraja hilo linalojengwa na wakandarasi China Civil Engineering Construction Corporation na China Railway 15 Group Corporation litaondoa adha ya usafiri wa wananchi, mizigo na magari ambayo kwa sasa huvushwa kwa vivuko, na kwamba baada ya ujenzi idadi ya magari yanayovuka kwa siku inatarajiwa kuongezeka kutoka 1,600 hadi 10,200 kwa siku na muda kuvuka utapungua kutoka saa 2:30 hadi dakika 4.
Akizungumza katika sherehe hizo, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Kanda ya Ziwa hususani Mikoa ya Mwanza na Geita kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo litakuwa utatuzi wa kero ya miaka mingi, iliyosababisha vifo kutokana na ajali za majini na wagonjwa kucheleweshwa hospitali, kuchelewa kwa biashara na safari za wananchi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Joseph Magufuli akikata utepe wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja refu zaidi Afrika Mashariki.
Mwonekano toka angani wa daraja la Kigongo - Busisi liltakavyokuwa likionekana litakapokamilika.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.